The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla y a Kifo-19

1

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA

Hatimaye msichana bilionea, Elizabeth anajitolea kumsaidia mtoto mgonjwa aliyepooza kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu. Ghafla, anajikuta akianza kumpenda kaka wa mtoto huyo. Unajua nini kilitokea? SONGA NAYO..

 Huo ndiyo ukawa mwanzo wa wawili hao kufahamiana. Hata Elizabeth aliporudi nyumbani, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mvulana aliyekutana naye hospitalini. Moyo wake ulikuwa kwenye mapenzi ya dhati, hakutaka kukumbuka tena kuhusu Edson, mwanaume aliyetokea kuuteka moyo wake kwa kipindi hicho alikuwa James.

Mara kwa mara bilionea kutoka nchini Uganda, Olotu alikuwa akimpigia simu lakini Elizabeth hakutaka kuipokea, mtu pekee aliyekuwa ameuteka moyo wake kwa kipindi hicho alikuwa James pekee.

Alikuwa kijana maskini ambaye hakuwa na kitu chochote kile, kwake, hakujali hata kidogo, alichokuwa akikiangalia moyoni mwake ni mapenzi tu. Japokuwa aliteseka sana usiku lakini hakujua kama mwanaume huyo angekubaliana naye au la, alichokitaka ni kujaribu bahati yake tu.

“Candy!” aliita simuni.

“Niambie shosti.”

“Nimeshindwa kulala.”

“Kisa?”

“James ananiumiza jamani, nimekaa nikimuwaza yeye tu,” alijibu Elizabeth.

“Jamani! Yaani kukutana naye leo tu umechanganyikiwa?”

“Mmmh! Shoga yangu wewe acha tu, ninateseka kwa mapenzi yake. Ninamtaka, natumaini atanikubalia,” alisema Elizabeth.

“Jaribu bahati yako,” alisema Candy.

Hilo ndilo alilolitaka, hakutaka kuona akipingwa, kila wakati alipofikia hatua ya kumwambia mtu yeyote kile alichokuwa akikihitaji alitaka kuona akiungwa mkono hata kama jambo lingekuwa baya kiasi gani.

Kwa Candy kumwambia kwamba alitakiwa kujaribu na angeweza kufanikiwa, akafurahi na kuahidi kufanya hivyo. Alichokifanya ni kwenda hospitali pale mara kwa mara, huko alikutana na James na kuzoeana naye ili baadaye ije kuwa rahisi hata kumwambia alichotaka kumweleza.

James hakuonekana kujali, alioneshwa ishara zote za kimapenzi lakini kutokana na msongo wa mawazo aliokuwa nao, hakuzigundua, yaani kwa Elizabeth ilionekana ni kama alikuwa akimuonesha kipofu ishara zile.

Baada ya wiki moja, kila kitu kilipowekwa tayari, safari ya kuelekea nchini India katika Hospitali ya Apollo iliyokuwa katika Jiji la Chennai nchini humo ikaanza. Baada ya saa ishirini, ndege binafsi ya Elizabeth ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chennai uliokuwa katika jiji hilo.

Mlango ukafunguliwa, tayari gari la kubeba wagonjwa la Hospitali ya Apollo lilikuwa limefika uwanjani hapo na hivyo kumbeba Glory aliyekuwa kitandani na moja kwa moja safari ya kuelekea hospitalini kuanza.

“Elizabeth! Hivi atapona kweli?” aliuliza James huku akionekana kutokuamini.

“Atapona tu, ninayaamini sana matibabu ya hapa, usijali James,” alijibu Elizabeth huku akimwangalia mwanaume huyo kwa macho yaliyojaa mahaba tele.

“Nashukuru kwa faraja yako.”

Walichukua dakika ishirini ndipo gari hilo lililokuwa likipiga king’ora likafika katika hospitali hiyo kubwa na kuingia ndani. Manesi ambao tayari walijiweka nje ya jengo la hospitali ile walipoliona gari hilo likiingia, wakaanza kusukuma machela kisha kuufungua mlango na kumteremsha Glory na kuanza kuisukuma machela ile ndani.

“Hatuwezi kuwa hospitalini hapa siku zote za matibabu, inatupasa tukachukue vyumba hotelini,” alisema Elizabeth.

“Hakuna tatizo!”

Huko ndipo Elizabeth alipotaka kumaliza kila kitu. Hakuwa radhi kuendelea kuvumilia zaidi na wakati moyo wake ulikufa na kuoza kwa mwanaume huyo, alichokuwa akikitaka ni kuona anakuwa mpenzi wake na kuendelea na maisha kama kawaida.

Kwa sababu tayari Elizabeth alikuwa amekwishaweka oda ya vyumba vya hoteli kubwa na ya kifahari ya Pentagon iliyokuwa katikati mwa Jiji la Chennai, walichokifanya ni kuchukua gari na kwenda huko ambapo vyumba vyao vilikuwa jirani.

“Hapa ndipo tutakapolala! Ushawahi kulala hotelini?’ aliuliza Elizabeth.

“Hapana!”

“Sawa! Baada ya hapa, turudi hospitali,” alisema Elizabeth.

Hapo ndipo walipopata muda wa kuoga na kujiandaa tayari kwa kurudi hospitalini. Chumbani, Elizabeth alikuwa na mawazo tele, kila alipokuwa akimwagikiwa na maji ya bomba la mvua, aliyainua macho yake juu kisha kukishikashika kifua chake hali iliyomletea mhemko mkubwa na kutamani kuwa na James mahali hapo.

Alikuwa kwenye wakati mgumu mno, hakutaka kuona akishindwa hata mara moja, alimhitaji sana James kwani moyo wake ulizizima kwa penzi la kijana huyo.

Je, Elizabeth atafanikiwa kumnasa James? Usikose wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

1 Comment
  1. ahadykidehele says
Leave A Reply