The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla Ya Kifo-18

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA…
Moyo wa bilionea Elizabeth unaguswa baada ya kumuona mtoto mdogo wa kike akiwa amepooza katika Hospitali ya Muhimbili. Hakuna anachokifikiria zaidi ya kumsaidia kwani alimuonea huruma, ila alitokea kumpenda mno.
SONGA NAYO…

Moyo wake uliguswa kumsaidia mtoto yule, kila alipomwangalia, alihisi maumivu makali moyoni mwake, msukumo mkubwa juu ya kumsaidia uliendelea kumsukuma moyoni mwake, huruma ilizidi kumuingia zaidi.

Candy alionekana kulishtukia hilo, alijua fika kwamba rafiki yake huyo alikuwa ameguswa na hali aliyokuwa nayo binti yule kwani kila alipomwangalia, Elizabeth alikuwa bize kumwangalia mtoto yule.
“Anahitaji kiasi gani kwa ajili ya matibabu?”
“Milioni saba!”

“Sasa atazipata kweli?”
“Mmmh! Nao huo ni mtihani mwingine japokuwa kaka yake anafanya michango mitaani.”
Katika maisha yake ya ubilionea alikuwa mtu wa kutoa msaada na kuamini kwamba kila alipoongezewa, ni kwa sababu alitoa sana. Mtoto yule aliyeonekana kuwa hoi, hakutaka kumuacha hivyohivyo, alijiona kuwa na kila sababu ya kuweza kumsaidia.
“Candy!”

“Abeee…”
“Nakuwa na msukumo wa kumsaidia binti huyu,” alimwambia Candy.
“Kweli?”
“Hakika!”
“Basi hakuna tatizo.”
Wakati wanazungumza hivyo, tayari lifti ikafika chini na kuteremka, hawakutaka kuelekea ndani ya gari, walichokifanya ni kufuatilia binti yule alikuwa akipelekwa wapi. Walipoona kwamba amepelekwa katika Wodi ya Mwaisela, wakaondoka zao na kuahidi wangerudi mahali hapo siku inayofuata.

Siku hiyo Elizabeth alikuwa akimfikiria mtoto yule tu, moyo wake uligubikwa kwa huzuni kubwa kiasi kwamba akakosa furaha kabisa, mawazo juu ya msichana yule mdogo yalikisumbua kichwa chake na kuahidi kuendelea kumfuatilia siku inayofuata ili ajue ni wapi alitakiwa kuanzia kwani kutokana na fedha alizokuwa nazo, milioni saba halikuwa tatizo lolote lile.

Siku iliyofuata aliamka asubuhi na mapema, kitu cha kwanza kabisa kilichokuja kichwani mwake ni kuhusu mtoto aliyekuwa amemuona siku iliyopita aliyemfanya kuwa na msukumo mkubwa wa kutaka kumsaidia kutokana na tatizo kubwa alilokuwa nalo, hakutaka kuchelewa, akaanza safari ya kwenda huko akiwa na Candy.

Kilichowakera ni foleni za barabarani. Walijikuta wakisimama muda mrefu kuliko kutembea. Ila pamoja na hayo yote, ndani ya dakika hamsini wakajikuta wakiwa kwenye jengo la hospitali hiyo ambapo waliteremka na kuanza kuelekea humo.
“Samahani,” alimwambia nesi mmoja.
“Bila samahani.”

“Nataka kufika katika Wodi ya Mwaisela.”
“Nendani kule mbele.”
Hawakutaka kusubiri, walichokifanya ni kuondoka na kuelekea huko. Si kwamba Elizabeth hakufahamu mahali ilipokuwa hiyo wodi, alifahamu vilivyo lakini kutokana na kuchanganyikiwa kwake, hakuweza kufahamu mahali ilipokuwa.

“Yule kule,” alisema Elizabeth na kuanza kuelekea alipoonyeshea kidole chake ambapo kulikuwa na nesi aliyekuwa akimshusha Gloria kutoka kitandani, japokuwa ndani ya wodi ile kulikuwa na wagonjwa wengi, ila wote walimuonea huruma Gloria.

Alipofika katika kitanda kile alichokuwa mtoto yule, Elizabeth akashindwa kuvumilia, hapohapo machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake, aliumia mno na hakuamini kama kulikuwa na watu waliokuwa wakipata mateso makali vitandani kama ilivyokuwa kwa mtoto yule.
Alibaki akiwa amesimama tu, japokuwa ndani ya wodi ile kubwa kulikuwa na watu wengi lakini hakukuwa na yeyote aliyeweza kugundua kama mtu aliyekuwa amesimama karibu na kitanda alichokuwa mtoto aliyepooza alikuwa Elizabeth.

Glory hakuweza kusimama na kwenda chooni, hapohapo alikuwa amewekewa mipira iliyomsaidia kujisaidia haja kubwa na ndogo ni manesi, tena wenye upendo wa hali ya juu ndiyo waliokuwa na jukumu kubwa la kubadilisha mipira ile kadiri ilivyokuwa ikitumika, tena kila baada ya siku mbili.
“Samahani nesi. Ninataka kumsaidia huyu mtoto asafirishwe kwenda kufanyiwa matibabu India…” alisema Elizabeth.

“Hakuna tatizo, unatakiwa kuwasiliana na daktari,” alijibu nesi yule.
“Nataka nimuone, unaweza kunipeleka sasa hivi?”
“Hakika!”

Je, nini kiliendelea? Fuatilia wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

Leave A Reply