The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla ya Kifo-22

1

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Safari ya kuelekea Ujerumani inaanza, njiani, James anakuwa na mawazo tele, haamini kama kweli leo hii ugonjwa wa mdogo wake umeshindikana mpaka kupelekwa huko. Njiani, muda wote anakuwa mtu wa kubembelezwa tu.
SONGA NAYO.

Ndege iliendelea kukata mawingu mpaka baada ya saa ishirini ilipoanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Munich nchini Ujerumani. Tayari gari la wagonjwa la Hospitali ya Rechts der Isar lilikuwa mahali hapo, walichokifanya ni kumshusha kisha kumuweka garini humo na safari kuanza.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika eneo la hospitali hiyo ambapo mlango wa gari ukafunguliwa, machela ikaletwa na kupandishwa kisha kuanza kusukumwa kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo.
Mara baada ya Glory kupelekwa katika chumba cha uchunguzi, jopo la madaktari saba likakutana ndani ya chumba kidogo kwa ajili ya kuizungumzia hali aliyokuwa nayo hata kabla hawajaanza kufanya upasuaji.
Wakaiweka mezani ile ripoti iliyotoka nchini India na kuanza kuipitia kwa ukaribu zaidi. Walitaka kujua tatizo lilianzaje na madaktari wa India walifanikiwa kwa kiasi gani. Wakaanza kuichambua ripoti ile.
“Uti wa mgongo umevunjika kidogo,” alisema Dk. Zeus.
“Unahisi tunaweza kutumia muda gani?”
“Mpaka apone?”
“Si chini ya miaka mitano.”
“Mmh!”
“Ndiyo hivyo! Hakuna kitu kibaya katika mwili wa binadamu kama kuvunjika uti wa mgongo, mpaka kurudi na kuwa kama zamani, huhitaji muda mrefu mno na wakati huo wote, chakula chake kikubwa kiwe kongoro kwa ajili ya kuurudisha uti huu katika hali yake ya kawaida,” alisema Dk. Zeus, daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo.
“Sawa!”
Hawakuwa na muda mwingi wa kupoteza, walichokifanya ni kuondoka chumbani mle na kuendelea na kazi zao. Moja kwa moja Dk. Zeus akawaita James na Elizabeth ndani ya ofisi yake na kuanza kuzungumza nao.
Hakuwaficha, aliwaambia ukweli kwamba japokuwa mgonjwa huyo aliletwa hospitalini lakini bado uhakika wa kupona kwa haraka chini ya miaka mitano ulikuwa mdogo mno. Walipoambiwa hivyo, kila mmoja akahuzunika, matumaini ya Glory kupona haraka iwezekanavyo yakapotea kabisa.
“Kwa hiyo tutatakiwa kusubiri kwa miaka mitano?” aliuliza James huku machozi yakijikusanya machoni mwake.
“Ndiyo!” alijibu Dk. Zeus.
Machozi yakaanza kububujika mashavuni mwa James. Aliendelea kuwa kwenye maumivu makali.
******
Rasheed alishtuka kutoka usingizini, kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kuchukua simu yake na kuangalia saa, ilikuwa ni saa tisa usiku. Uso wake ulijawa na tabasamu pana, ndoto aliyokuwa ameiota kipindi kifupi kilichopita ilimfanya kuwa na furaha mno.

Aliota akiwa na msichana mrembo mno, msichana aliyemfahamu ambaye alikuwa naye siku chache zilizopita, Elizabeth. Kwenye ndoto hiyo aliota akiwa naye sehemu fulani ambayo hakujua ilikuwa sehemu gani, walikuwa na furaha mno na muda wote walikuwa wakibusiana kwa furaha, walishikana mikono na kuzunguka huku na kule na kila aliyewaangalia, aliyaona mapenzi mazito yakiwazunguka.
Kama njiwa, walikuwa wamekumbatiana muda wote, kila kitu kilichokuwa kikiendelea kiliwapa furaha mno. Wote walikuwa mabilionea na wote walikuwa na mioyo iliyojaa mapenzi kiasi kwamba hakukuwa na mtu ambaye angewatenganisha.
Ndoto hiyo ikampa mawazo mengi, akaanza kumkumbuka msichana huyo ambaye kipindi cha nyuma wala hakuwa kabisa mawazoni mwake.

Ilipofika saa tisa alasiri, akashindwa kuvumilia, hapohapo akajikuta akichukua simu yake na kumpigia Elizabeth kwa lengo la kuwasiliana naye. Alipojaribu kupiga simu, haikuwa ikipatikana kitu kilichomfanya kuwa na mawazo tele.
Hakutaka kukubali hata mara moja, alichokuwa akikifikiria ni kwamba inawezekana alikuwa amepumzika hivyo alizima simu yake, alichokifanya ni kuvumilia, ilipofika saa kumi akampigia tena lakini majibu yalikuwa yaleyale, simu haikuwa ikipatikana.

Akashikwa na mawazo mengi, akakosa raha kabisa, kila alipokuwa akimpigia simu majibu yaliendelea kuwa yaleyale kwamba simu haikupatikana. Alichokifanya ambacho aliona kisingekuwa na tatizo lolote lile ni kumtumia barua pepe ili kama hakuwa nchini Tanzania basi aweze kuipata.
Katika barua pepe hiyo alimwambia kwamba alitaka kuonana naye, alikuwa akitamani kuzungumza naye na hivyo ingekuwa vizuri kama wangekutana sehemu na kuzungumza.
“Kwa sasa ni ngumu,” alijibu Elizabeth, hapohapo Rasheed akajua kwamba mwanamke huyo alikuwa ‘online’.
Kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

1 Comment
  1. Aman Norbety says

    Huwaga sehemu yenye vitendo vya utamu wa Wahusika hauonyeshwi bwana ndy maana wana2nyima raha

Leave A Reply