The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla ya Kifo

0

“Kwani inahusu?”

“Subiri kwanza…usipaniki Elizabeth, kuna swali nataka kukuuliza.”

“Nimesema sihitaji maswali.”

“Lakini Elizabeth! Unajua Tanzania inakuheshimu sana, sasa imekuwaje mpaka ukavaa vile? Tena mbele za watu, watoto wote Tanzania walikuwa wakiangalia kipindi kile, ukajianika tu na vivazi vyako vya uchuro”

“Kwani kuna tatizo? Mbona nyie mnakuwa washamba sana, mbona akina J.Lo hamuwaambii? Juzikati Kim Kardashian alivaa vilevile, mlimwambia? Au kisa amefanya Elizabeth? Hebu nitolee uchuro wako huo, kama hauna hela, sema nikupe, kama hauna cha kuandika, kaandike kuhusu mama yako,” alisikika msichana mrembo Elizabeth, baada ya kutamka maneno hayo, akaingia ndani ya gari lake la kifahari, Ferrari 458 Spider lenye gharama zaidi ya milioni mia nne na kuondoka zake.

Elizabeth Dickson Marcel alikuwa mwanamitindo aliyekuwa na jina kubwa barani Afrika, alifanikiwa zaidi, alibuni mavazi yake mwenyewe na kuyasambaza nchi mbalimbali duniani kiasi kwamba akatengeneza jina na kumfanya kuwa maarufu mkubwa hata zaidi ya mwanamke yeyote yule barani Afrika.

Mara kwa mara alikuwa mtu wa kuonekana kwenye magazeti, maisha yake yaliyojaa vituko yaliwashangaza watu wengi kiasi kwamba hawakujua kitu alichokitafuta kwani kama jina kubwa, alikuwa nalo, kama ni fedha, alikuwa nazo za kutosha kabisa na kumfanya kuwa bilionea.

Waandishi wa habari hawakumuacha, japokuwa kila siku alisema kwamba anachukia kufuatiliwa na waandishi hao lakini waliendelea kumfuatilia, kila walipomuona baa akinywa na mwanaume, habari yake iliandikwa, walipomuona akiingia kwenye gari la mwanaume mwingine, pia habari hiyo ikaandikwa.

Japokuwa hakuishiwa vituko, lakini Elizabeth alitokea kupendwa mno, watu walimheshimu kwa kuwa alikuwa mtafutaji sana, kichwa chake kilikuwa na akili ya kutafuta fedha, kila alipokaa, alifikiria fedha na hata wanaume alikuwa akitoka nao kimapenzi, ni wale waliokuwa na fedha tu ambao aliamini wangeweza kumpa njia nyingi za kutafuta fedha.

Alikuwa mwanamke maarufu kuliko wote barani Afrika, kupitia umaarufu wake bado alikuwa akitengeneza kiasi kikubwa cha fedha na kumfanya kuwa mwanamke mwenye fedha ndefu kuliko wote barani Afrika.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply