Penzi la kweli lina historia hakikisha

MUNGU ni mwema sana mpenzi msomaji. Ametukutanisha tena Jumamosi nyingine ili tuweze kupata elimu mpya ya masuala ya uhusiano.

Hakuna sababu ya kuwa mbishi. Ukiruhusu moyo wako kujifunza, utajifunza na kuweza kubadilika katika maeneo ambayo haukuwa sawa kwani hakuna mwanadamu aliyekamilika.

Wiki iliyopita tulijifunza kuhusu umuhimu wa wapendanao kupeana. Nilisema, utamu wa penzi ni wapendanao kushirikiana. Ukiona mwenzako anakujali, huna budi na wewe kumjali. Akikutendea kitu kinachokupa faraja, jitahidi na wewe umpe faraja.

Kila mtu anakuwa na kitu anachokipenda. Ukiona mwenzako amekufanyia kitu unachokipenda, na wewe mpe kile anachokipenda. Mapenzi yatanoga kwelikweli.

Mtaishi kwa amani kwani kila mmoja wenu anajitahidi kwa hali na mali kumpa faraja mwenzake. Hayo ndiyo mapenzi ya kweli. Tofauti na hapo, wizi mtupu!

Tukirudi katika mada ya leo, ni vyema kutambua kwamba penzi lolote lililopata kufanikiwa duniani mara nyingi linakuwa na historia yake. Unawezaje kuitengeneza historia hiyo? Twende pamoja katika darasa hili la leo na nina imani utajifunza kitu.

Vijana wengi sasa hivi wanajikuta wakirukaruka kwa sababu hawataki kutengeneza historia. Wenyewe wanasema eti hawataki usumbufu. Hawataki sarakasi za kila uchwao. Akiingia kwenye uhusiano anataka kila kitu kiwe sawa.

Hataki kukuta mwenzake ametofautiana naye baadhi ya vitu. Mfano mwenzake anaweza kuwa mvutaji wa sigara, basi akigundua tabia hiyo inamkera, anavunja uhusiano haraka kama shoti ya umeme. Hana muda wa kumbadilisha mwenzake, anasema; ‘hanifai, acha niendelee mbele kwa mbele’.

Huo ni mfano mdogo tu wa tabia. Zipo nyingi zinazofanana na hiyo. Hivyo atatoka kwa huyu na kuhamia kwa mwingine na akikuta nako kuna kitu hakiendi sawa, anafungasha virago na kuhamia kwa mwingine akijipa moyo kuwa bado Mungu hajamuandikia.

Kwamba ipo siku atampata mtu ambaye wataendana kwa kila kitu. Watafanana kwa kila kitu, yaani yupo mmoja ‘spesho’ ambaye ameumbwa kwa ajili yake. Kwingine kote anafanya mazoezi kama vile ‘twisheni’ na mtihani unakuja.

Ndugu zangu, tunajidanganya. Hakuna kitu kama hicho. Kama unataka kitu kizuri, kitengeneze. Kama unataka kufikia kilele cha mafanikio na mwenzako, kipimo chake kikubwa ni historia. Tengeneza historia na mwenzako na baadaye mtafikia mahali nyinyi wenyewe mtasema; ‘Ni Mungu tu, sisi tulikuwa si wa kufika hapa.’

Ukichunguza kwa makini, wapendanao wengi ambao sasa wanaishi kwenye ndoa watakwambia, haikuwa kazi rahisi. Walipambana. Waliruka viuzi vya kila namna. Wakikuelezea mapito yao huwezi amini. Utapigwa na butwaa, wenye moyo mwepesi hawawezi.

Kwa ambaye hapendi usumbufu, huishia kutangatanga, leo huku kesho kule. Huwezi kuwa mtu wa kurukaruka kila siku halafu utegemee kwamba utafikia kilele cha mafanikio. Jitahidi kadiri uwezavyo kuwa mvumilivu.

Kuwa mnyenyekevu kwa mwenzako. Vumilia udhaifu wa mwenzako maana kila binadamu ana upungufu wake.

Mwenzako amekosea kitu katika safari yenu, usifanye uamuzi kwa hasira. Chukulia ni changamoto. Hakuna waliofanikiwa bila changamoto. Jifunze kutokana na changamoto hizo ndipo utatengeneza historia ya kweli.

Kama ni kugombana, gombaneni kwelikweli. Kama imetokea mwenzako ameonesha udhaifu kwa mwanamke mwingine, usikimbilie kumuacha. Suala la kukata tamaa liwe la mwisho. Hakikisha unatumia akili na busara kadiri Mungu alivyokujalia.

Ukiona mwenzako amekasirika, hata kama yeye ndiye mkosaji. Shuka chini na uweze kumuelezea tatizo lake kistaarabu. Mueleze kwamba anapaswa kukuheshimu wewe kwani ndiye mwenzake mliyepanga kufika mbali.

Kama ni muungwana na ana dhamira ya dhati, hakika ataelewa. Atakuwa mpole na kukuomba radhi. Msamehe na umpe nafasi nyingine ya kuendeleza safari yenu.

Usikubali kirahisi kuahirisha safari. Ianze upya kadiri uwezavyo. Leo mtagombana, mtapatana na kuanza safari upya. Ikitokea tena mmegombana, usichoke. Endelea kupambana hadi mwisho wa kutengeneza historia.

Ukizingatia hayo, hakika penzi lenu litafikia wakati litakuwa na historia kubwa ambayo mtakuwa mmeitengeneza nyinyi wenyewe, mtapongezana na maisha yatazidi kuendelea!

Toa comment