Penzi la Mobeto na Fred Lafunika Harmo, Kajala

UNAAMBIWA moto wa penzi jipya la mwanamama Hamisa Mobeto na mfanyabiashara maarufu Bongo, Fred Vunjabei limelifunika vibaya lile la Rajab Abdul ‘Harmonize’ na mwanamama Kajala Masanja.
Penzi la Mobeto na Fred linatajwa kushika kasi ya ajabu baada ya wawili hao kutofanya siri tena.
Habari za ndani kabisa ambazo Gazeti la IJUMAA limepenyezewa zinadai kuwa, baada ya Mobeto kuona penzi la Kajala na Harmonize au Harmo ndilo linalotrendi zaidi na kushika vichwa vya habari, basi na wao wameamua liwalo na liwe ambapo kwa sasa wanajiachia waziwazi bila kificho kama mwanzo.

Wakati Harmona Kajala wakiwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Mobeto na Fred nao walionekana wakijiachia kwenye hoteli moja ya kitalii jijini Arusha huku wakiwa hawana habari tena na watu ambao wanawajadili kila kukicha.
Kujiachia kwao kumewafanya baadhi ya watu walikuwa hawaamini kama ni wapenzi kupigia mstari kwani hawana siri tena.
“Mimi nipo nao huku Arusha, wenyewe wanajiachia tu, hawana hawana hata habari.“Kuna sehemu tulikuwa hukuhuku Arusha, watu wakawa wamewazunguka, wanawashangaa, lakini wao wakawa wako bize na mambo yao,” anasema mmoja wa mashuhuda walioambatana na timu ya Mobeto na Fred kwenda jijini Arusha wikiendi iliyopita.
Mpashaji wetu huyo anasema kuwa, pamoja na kwamba Fred anaonekana kuona aibu anapokuwa na Mobeto mbele za watu, lakini kwa Mobeto ni tofauti kwani anaonekana ni mwenye furaha na anajiachia mpaka basi, bila kujali chochote kile wala kuwaza mitandao ya kijamii itasema nini.
“Watu wengi walikuwa wakijiuliza, Mobeto mbona amekuwa jasiri sana kwenye uhusiano huu, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma?“
Lakini kwa ufupi kila mtu anayewaona anafurahia uhusiano huu,” anasema kikulacho mmoja ambaye ni mtu wa karibu wa wawili hao.
Gazeti la IJUMAA lilizungumza na Mobeto kujua anajisikiaje kwenye uhusiano wake huo mpya na Fred na kwamba mashabiki wake watarajie nini ambapo alisema kuwa, angefurahia zaidi kama watu wangetamani kujua juu ya kazi zake badala ya kutaka kujua kuhusu yeye binafasi.
“Mimi ninawaomba watu kufuatilia zaidi kazi zangu zinazozifanya kuanzia mitindo, mavazi, muziki na vingingine vingi ninavyofanya kwenye jamii, hayo mengine hayatawasaidia sana,” anasema Mobeto ambaye ni mama wa watoto wawili aliozaa na Majizo na Diamond Platnumz.
STORI: IMELDA MTEMA, DAR

