Penzi lisiloisha (Unending Love)-042

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanashangazwa mno na hali duni na umaskini uliokithiri wanayoikuta nyumbani kwa akina Jafet. Wanarejea jijini Mwanza na siku zinazidi kusonga mbele, hatimaye vijana hao wanahitimu kidato cha sita lakini mama yake Anna hampendi tena Jafet na anafanya kila kinachowezekana kuwatenganisha wawili hao.

Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Mimi si nilikwambia ukawa huamini mwanangu? Hakuna mapenzi kati ya maskini na tajiri, kama ni mke wa kuoa umri wako ukifika utachagua maskini mwenzako hapahapa kijijini utamuoa, wala huna sababu ya kung’ang’ania mambo makubwa usiyoyaweza,” alisema mama yake Jafet.

Japokuwa alikuwa akimpa maneno ya kumtia nguvu, ndani ya moyo wake na yeye aliumia mno kwa kilichotokea hasa kutokana na ukweli kwamba Jafet alikuwa amejitolea figo kwa ajili ya kumsaidia msichana huyo.

“Siku nyingine utaona umuhimu wa kuwashirikisha wazazi wako katika mambo makubwa kama haya. Uliwezaje kumuamini mwanamke kiasi cha kufikia hatua ya kwenda kumpa figo yako bila hata kutushirikisha sisi wazazi wako? Mambo mengine Mungu anakuonesha hapahapa duniani,” alisema mama Jafet, kauli ambayo ilimfanya kijana huyo mdogo aanze upya kuangua kilio.

Kila alipokuwa akifikiria jinsi alivyojitolea kwa ajili ya msichana huyo, aliona kabisa kwamba hastahili kulipwa mabaya kiasi hicho, huzuni ikaendelea kuyagubika maisha yake.

Siku zilizidi kusonga mbele huku Jafet akiendelea kudhoofika kutokana na mawazo juu ya Anna. Hakuwa na uwezo wa kula vizuri tena, kulala wala kufanya mambo mengine ya msingi kama ilivyokuwa awali, hali ambayo ilimsikitisha kila mtu pale nyumbani kwao.

Japokuwa baba yake alikuwa mlevi na mkali sana kwa mwanaye, naye alijikuta akiguswa kama mzazi, siku nyingine akawa anajaribu kukaa na Jafet na kumpa ushauri nasaha wa namna ya kukubaliana na hali halisi ya kilichotokea.

Hatimaye matokeo ya kidato cha sita yalitangazwa ambapo kama kawaida, Jafet alifaulu kwa kiwango cha juu na kupata daraja la kwanza (division one). Kilichozidi kumtia uchungu, ni kuona kuwa hatimaye juhudi zake za kumfundisha Anna zilikuwa zimezaa matunda kwani matokeo yalionesha kuwa msichana huyo amepata daraja la pili (division two).

Kila mtu aliyekuwa anamfahamu Anna, alijua kwamba msichana huyo asingeweza kufaulu kwa kiwango hicho bila msaada mkubwa wa Jafet kwani alikuwa akijitahidi kumuelekeza na kumfundisha kila siku, muda mwingine akilazimika kutumia hadi muda wa ziada mpaka msichana huyo aelewe.

“Sina cha kusema Anna, Mungu atanilipia kwa wema wangu kwako, nilijitoa kwa kila kitu, sikutaka kuona unapata shida, nilijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu lakini leo umenilipa kwa kuniachia jeraha ndani ya moyo wangu ambalo kamwe halitakuja kupona, nakushukuru sana mpenzi wangu,” alisema Jafet akiwa kwenye chumba cha ‘internet cafe’, mjini Geita, muda mfupi baada ya kumaliza kuangalia matokeo.

Japokuwa alikuwa amefaulu, kila mtu alimshangaa alivyokuwa analia kwa uchungu huku akizungumza peke yake kama mwendawazimu. Alipoona watu wanamshangaa sana, alitoka na kufunga safari ya kurejea kijijini kwao, Rwamgasa.

“Vipi matokeo yamekuwaje? Halafu mbona kama ulikuwa unalia?” mama yake Jafet alimuuliza mwanaye, muda mfupi baada ya kurejea kutoka mjini kuangalia matokeo.

“Nimefaulu mama, nimepata ‘divisheni wani’, namshukuru Mungu.”

“Oooh! Hongera sana mwanangu, mi nilijua tu lazima utafaulu. Sikuzaa mtoto asiye na akili mimi,” alisema mama Jafet kwa furaha na kumkumbatia mwanaye huyo kwa furaha, lakini akashangaa kumuona anaanza upya kuangua kilio.

“Mbona unalia mwanangu? Kuna tatizo?”

“Nalia kwa furaha mama, nimefurahi sana kufaulu,” Jafet alidanganya kwani kiukweli kilichokuwa kinamliza ilikuwa ni kumbukumbu za Anna.

***

Anna alikuwa amekaa kwenye bustani za chuo, akipiga stori za kawaida na rafiki yake mpya, William Mbawala, ghafla simu yake ikaanza kuita. Alipogundua kwamba ni baba yake alikuwa anampigia, ilibidi amuage William na kuondoka haraka eneo hilo, akaipokea simu hiyo ambapo baba yake alimtaarifu kwamba matokeo ya kidato cha sita yameshatoka.

Kutokana na shauku aliyokuwa nayo, moja kwa moja alienda kwenye ‘internet cafe’ ya chuoni hapo na kuingia kwenye mtandao ambapo hakuyaamini macho yake alipogundua kwamba amefaulu kwa kiwango cha daraja la pili, akapiga kelele kwa furaha.

Hata hivyo, furaha hiyo ilidumu kwa muda mfupi tu. Kama ilivyokuwa kwa Jafet na kama ilivyokuwa kwa kila mtu aliyekuwa anafahamu uwezo wake darasani, Anna alijua kwamba bila jitihada za nguvu za Jafet, kamwe asingeweza kufaulu kwa kiwango hicho. Kumbukumbu za Jafet zikawa zimerejea upya ndani ya kichwa chake, akaanza kulia kwa uchungu na kukimbilia kwenye hosteli aliyokuwa anaishi, akajifungia.

“Naendelea kukuomba msamaha Jafet, nilitamani ningekuwa karibu tushangilie pamoja ushindi huu lakini nasikitika kwamba nipo mbali, hayakuwa malengo yangu kuondoka na kukuacha kwenye hali hiyo, bado nakupenda mwenzio,” alisema Anna huku akiwa analia.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.


Loading...

Toa comment