The House of Favourite Newspapers

Penzi lisiloisha  (unending love)- 40

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanashangazwa mno na hali duni na umaskini uliokithiri wanayoikuta nyumbani kwa akina Jafet. Wanarejea jijini Mwanza na siku zinazidi kusonga mbele, hatimaye vijana hao wanahitimu kidato cha sita lakini mama yake Anna hampendi tena Jafet na anafanya kila kinachowezekana kuwatenganisha wawili hao. Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Jafet hakuacha kumfikiria Anna, kila siku mawazo yake yalikuwa kwa msichana huyo aliyempenda kwa dhati. Japokuwa hakutaka kumuonyeshea mama yake jinsi alivyokuwa na huzuni lakini hilo lilishindikana, huzuni yake haikuweza kufichika.

Siku ziliendelea kukatika mpaka ikafika siku ambayo alishindwa kuvumilia, hakutaka tena kukaa kijijini Rwamgasa kitu kilichomfanya kupanga safari ya kuelekea jijini Mwanza kwa ajili ya kuonana na Anna kwani bado hakuwa akipatikana katika simu.

“Ni lazima niende Mwanza, siwezi kuvumilia, siwezi kuendelea kuishi pasipo kumuona Anna,” alisema Jafet.

Alidhamiria kuondoka kijijini hapo na kuelekea jijini Mwanza, hakutaka kuendelea kubaki tena huko, jinsi alivyoumia moyoni, jinsi mawazo yalivyomkaa kichwani mwake, hakuona kama angeweza kuvumilia kukaa kijijini pasipo kwenda jijini Mwanza.

Siku iliyofuatia alikuwa ndani ya basi, alikaa katika kiti cha watu wawili, ingawa pembeni yake kulikuwa na abiria mwingine lakini tangu anaingia ndani ya basi hilo, hakutaka kuzungumza naye zaidi ya kumsalimia tu kisha kubaki kimya huku mawazo juu ya Anna yakiendelea kumjaa.

Kutoka Geita mpaka Mwanza Mjini, basi lilitumia saa nne, lilipofika, harakaharaka akateremka na kuanza kutoka nje ya kituo huku akiwa na begi lake dogo mgongoni. Safari yake haikuishia hapo, alianza safari nyingine ya kuelekea katika mtaa wa watu wenye fedha, Capri Point ambapo baada ya kufika huko akaanza kulifuata jumba la kifahari lililokuwa katikati ya mtaa huo.

“Karibu Jafet,” mlinzi alimkaribisha Jafet.

“Asante sana, Anna yupo?”

“Mmmh! Swali gumu! Hebu ingia kwanza.”

Hakutaka kubaki hapo nje, alichokifanya ni kuingia ndani. Kitendo cha mlinzi kutoa mguno mara baada ya kuulizia uwepo wa Anna ndani ya nyumba ile ulimtia shaka moyoni, akahisi mapigo ya moyo wake yakianza kudunda kwa nguvu huku kwa mbali kijasho chembamba kikiaanza kumtoka.

Alipoingia ndani, akapelekwa mpaka sebuleni ambapo baada ya kutulia kochini, dakika tano baadaye mama Anna akatokea sebuleni pale, alipomuona Jafet, kwa mbali akaonekana kushtuka.

“Anna yupo?” alimuuliza mwanamke yule mara baada ya salamu.

Mama Anna hakujibu swali hilo, alilisikia lakini akabaki kimya. Akaanza kumwangalia Jafet, japokuwa kijana huyo alisaidia kuokoa maisha ya binti yake kwa kumpa figo moja lakini mapenzi yake hayakuwa kwa Jafet hata kidogo.

Alimchukia, hakumpenda hata kidogo, maisha ya kimasikini aliyokuwa nayo yalimfanya kukosa thamani kwa mwanamke huyo kiasi kwamba kuna kipindi aliona kwamba binti yake hakutakiwa kuwa na mtu kama Jafet, maisha yao yalikuwa tofauti na kijana huyo.

“Umemuona tangu umeingia?”

“Hapana mama ndiyo maana nimeuliza.”

“Hayupo, ametoka!”

“Amekwenda wapi?”

“Sijui amekwenda wapi na sijui atarudi lini,” alijibu mwanamke huyo kwa sauti iliyoonyesha kwamba hakutaka maswali zaidi.

Mama Anna alibadilika, hakuwa kama alivyokuwa kipindi cha nyuma ambacho binti yake alikuwa akihitaji msaada mkubwa. Maswali mengi yakaanza kumiminika kichwani mwa Jafet juu ya mabadiliko ya mwanamke yule lakini jibu pekee lililomjia kichwani ni kwamba umasikini wake ulikuwa chanzo.

Hakutaka kubaki mahali hapo, moyo wake uliumia mno, alishindwa kuvumilia, alichokifanya ni kuaga. Mama Anna hakuongea kitu, alichokifanya ni kusimama na kuelekea chumbani mwake, Jafet hakujali, akatoka sebuleni pale na kuelekea nje.

“Amekwambia alipokwenda?” aliuliza mlinzi.

Hata kabla Jafet hajatoa jibu, honi ikaanza kusikika kutoka nje ya jumba hilo, alichokifanya mlinzi tena kwa haraka sana ni kulifuata geti na kulifungua, gari la kifahari la baba Anna likaanza kuingia mahali hapo, Jafet alibaki akiwa amesimama tu akiliangalia gari lile mpaka lilipokwenda kuegeshwa na baba Anna kuteremka.

“Nimekuja kumuona Anna,” alisema Jafet baada ya salamu, alizungumza kwa sauti ya kinyonge.

“Anna ameondoka kuelekea nchini Marekani. Nimempeleka katika chuo kimoja huko. Sidhani kama atarudi leo au kesho, nadhani atachukua zaidi ya miaka mitatu,” alisema baba Anna huku kwa mbali uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana ambalo lilikuwa kama msumali wa moto moyoni mwa Jafet.

***

Anna hakuwa na raha, moyo wake uliumia mno, kila kitu kilichoendelea katika maisha yake alihisi kama yupo ndotoni ambapo baada ya dakika kadhaa angeamka na kujikuta nchini Tanzania.

Hakuacha kumfikiria Jafet, moyo wake ulikosa furaha, kila alipokaa, iwe chumbani au darasani, hakuacha kumfikiria Jafet ambaye alimuingiza katika maisha ya kimapenzi.

Alitamani kuisikia sauti yake, hakujua ni kwa jinsi gani angelifanikisha hilo. Alikuwa na namba ya simu ya mvulana huyo lakini aliipoteza katika mazingira ya kutatanisha na hata alipojaribu kuitafuta kila kona, hakuweza kuipata.

Kama ni mateso, kipindi hicho yalikuwa makubwa, kuna kipindi alijuta kwenda nchini Marekani na kitu kilichomuumiza zaidi ni kwamba hakuwa amemuaga Jafet. Kilio chake, huzuni yake hazikuweza kubadilisha kitu chochote kile, kila kitu kilibakia kama kilivyokuwa kwamba mpaka anaingia nchini Marekani na wiki ya kwanza kukatika, hakuwa amemuona Jafet kitu kilichomuumiza mchana na usiku.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia kwenye gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.

Leave A Reply