pep: tuko kwenye wakati mgumu, tuna wachezaji 13
Kocha wa Machester City, Pep Guardiola (53) amesema kikosi chake kimebakiwa na wachezaji 13 kufuatia wachezaji wawili wa klabu ya klabu hiyo kupata majeraha hapo jana katika mchezo wa Kombe la Carabao dhidi ya Tottenham Hotspur na kushindwa kuendelea na mchezo huo uliomalizika kwa ushindi wa goli 2-1 kwa wenyeji Tottenham na kusonga hatua ya robo fainali.
Katika mchezo huo, beki Manuel Akanji alishindwa kutumika katika kikosi hicho baada ya kupata tatizo la misuli ya miguu katika mazoezi mepesi kabla ya mchezo kuanza, huku mshambuliaji Savinho akitolewa nje dakika ya 63 ya mchezo huo baada ya kupata jeraha katika kifundo cha mguu.
Pia kocha huyo amesema sababu ya beki kitasa Ruben Dias kushindwa kuendelea na mchezo huo kipindi cha pili ni maumivu yaliyokuwa yakimsumbua mara kwa mara.
“Tuna wachezaji 13, tuko kwenye kipindi kigumu kweli. Vijana wanaocheza, wanamaliza wengi wao kwa matatizo na tutaona jinsi watakavyopona. Nadhani tuko taabani, kwa sababu katika miaka tisa hatujawahi kuwa katika hali hiyo na majeraha mengi. Wachezaji hawa wanapiga hatua mbele, pamoja zaidi kuliko hapo awali, na tutajaribu kufanya hivyo wiki hii katika muda huu mfupi wa kupona” alisema kocha huyo raia wa Uhispania baada ya mchezo wa jana.
Man City sasa italazimika kuchukua baadhi ya wachezaji katika akademi yao na timu za vijana kwani katika kikosi hicho kwa wachezaji wanaocheza nafasi za mbele yaani kuanzia nafasi ya beki hadi mshambuliaji wanaopatikana ni Nathan Aké, Rúben Dias, Josko Gvardiol, Rico Lewis, John Stones, Josh Wilson-Esbrand (ambaye hajacheza mchezo wowote hadi sasa), Phil Foden, Ílkay Gündogan, Mateo Kovacic, James McAtee, Matheus Nunes, Bernardo Silva na Erling Haaland.