visa

Petit, mkewe wamwagana!

KAMA ulikuwa unasikiasikia tu bila kuwa na uhakika, habari ikufikie ni rasmi sasa, meneja wa wasanii, Ahmed Ngahemela ‘Petit Man’ amemwagana na mkewe Maimuna Adam ‘Queen Mai’, Risasi Jumamosi linakupa mchapo kamili. Ubuyu huu ulianza kusambaa kwa kasi kama moto wa kifuu mapema wiki hii ambapo taarifa zilieleza tu kwamba, Petit amerejesha majeshi kwa mzazi mwenziye Esma.

Mbali na ubuyu huo wa mitandaoni, Risasi Jumamosi lilimegewa taarifa hiyo kutoka kwa chanzo kilicho karibu na familia ya Petit. “Fuatilieni, mbona muda kidogo Petit na mkewe wameshaachana, kila mmoja yupo na hamsini zake. Hata kwenye ile bethidei ya Aunt, Mai alienda kivyake ili kuwapa sapoti mashosti zake kina Aunt na Wema,” kilisema chanzo hicho.

Aidha, chanzo hicho kilidokeza kuwa, baada ya kumwagana na mkewe huyo imekuwa rahisi kurejesha majeshi kwa Esma kama ambavyo sheria ya ndoa ya dini ya Kiislam inataka kwamba ukimpa mtu talaka tatu, huwezi kumrudia mpaka pale mmoja wenu atakapooa au kuolewa na mtu mwingine kisha kuachana naye.

“Karudi kwa Esma na kama unavyojua sheria ya ndoa ya dini ya Kiislam inavyotaka kwamba huwezi kumrudia mtu uliyempa talaka tatu mpaka pale utakapooa au mkeo kuolewa kisha kuachika au mwanaume kumuacha aliyemuoa,” kilisema chanzo.

Risasi Jumamosi lilijaribu kumtwangia simu Petit lakini simu yake iliita bila kupokelewa, lakini bahati nzuri Mai alipatikana na kukiri kuwa ndoa yao imeshavunjika. “Yeah ni kweli tumeshaachana lakini kuhusu kurudiana na Esma, mimi hayo hayanihusu,” alisema Mai bila kufafanua kama amepewa talaka na kama amepewa ni ngapi.

Alipoulizwa haoni kama ni mapema sana kwa wawili hao kuachana, alisema hilo yeye hajali kwani si wa kwanza kuachika. “Hiyo haijalishi kama tumekaa muda mfupi au mrefu, kwani kuachana ni mambo ya kawaida na mimi siyo wa kwanza kuachika,” alisema Mai.

Risasi Jumamosi pia lilipokuwa kwenye mizunguko yake ya kihabari juzikati, lilimfuma Esma akiwasiliana kimahaba na Petit kupitia ‘video call’. Esma alionekana kutoa ushirikiano kama wote kuonesha kwamba sasa mambo ni moto lakini hata hivyo alijihami kwa kuwataka waandishi waache kuulizia ubuyu huo.

“Nyie hapo nawajua, ole wenu muifanye hii kuwa habari. Tuongee mambo mengine kama mnataka,” alisema Esma. Mapaparazi wetu walipotaka kumbana zaidi, Esma hakutaka kufunguka kuhusu suala hilo, badala yake alitoa ushirikiano kwa habari nyingine tofauti na hiyo.

Esma na Petit waliachana kwa talaka tatu mwanzoni mwaka 2016, huku wakiwa tayari na mtoto mmoja. Hivyo kwa mujibu sheria ya Kiislam ya ndoa, kama wawili hao wamerudiana na wana mpango wa kufunga tena ndoa, sheria inawaruhusu.

Imeandaliwa na Memorise Richard, Irene Marango na Khadija Bakari.
Toa comment