Kartra

Pialali Vs Tinampay… Lazima Mtu Akae – Video

 

Mhariri Mtendaji wa Global Publishers na mchambuzi maarufu wa masuala ya michezo hapa nchini, Saleh Ally ‘Jembe’ (katikati) akiwatambulisha; Bondia Eduardo Mancito kutoka Ufilipino (kushoto) na Bondia wa Tanzania, Salim Mtango (kulia) wakati mabondia hao walipowasili katika ofisi za Global Group, Sinza Mori jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya utambulisho wa pambano lao watakalocheza Jumamosi, Novemba 28, 2020.

 

KUELEKEA pambano kali la kimataifa la ngumi kati ya Bondia Mtanzania, Idd Pialali ‘Simba’ na Mfilipino Arnel Tinampay, mambo yamepamba moto, ambapo mabondia hao kila mmoja ametamba kuhakikisha anamkalisha mpinzani wake mapema tu kwenye pambano hilo litakalofanyika Novemba 28, mwaka huu kwenye ukumbi wa Next Door Arena jijini Dar es Salaam.

Mabondia hao leo walipata nafasi ya kutembelea ofisi za Global Publishers na kufanya mahojiano kupitia kipindi maalumu cha +255 Global Radio yaliyoruka mubashara kupitia Global TV Online.

Bondia Arnel Tinampay kutoka Ufilipino (kushoto) na Bondia wa Tanzania, Idd Pialali (kulia) wakitambiana wakati mabondia hao walipowasili katika ofisi za Global Group, Sinza Mori jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya utambulisho wa pambano lao watakalocheza Jumamosi, Novemba 28, 2020.

Akizungumza na Championi Jumatano, Pialali alisema: “Nawaomba mashabiki wa ngumi wajitokeze kwa wingi siku ya Jumamosi ili kuja kushuhudia burudani ya kutosha niliyowaandalia.

 

“Nataka niwahakikishie kuwa hapa hakuna ushindi wa pointi ni lazima mtu akae kwa KO mapema tu ili wasije wakatuzoea, hivyo nimejiandaa kumchakaza mapema huyu Mfilipino.”

Naye Tinampay akijibu tambo hizo alisema: “Natamani mashabiki wangu waanze kutangulia pale Next Door Arena leo hii kwa sababu kuna sapraizi ya burudani ya kutosha kwa ajili yao nimeiandaa.

“Najua Pialali ni bondia mzuri lakini tayari nimemsoma na haitakuwa ngumu kumpiga.”

Pambano hilo limedhaminiwa na Gazeti la Spoti Xtra, +255 Global Radio, DSTV, Plus TV, Precission Air, Smart Gin, Kebby’s Hotel na Uhuru FM ambapo pia siku hiyo litashuhudiwa pambano jingine la kimataifa kati ya bondia Mtanzania, Salim Mtango kutoka Tanga ambaye atapanda ulingoni kuzichapa na Eduardo Mancito wa Ufilipino.

Kwa upande wa Mtango yeye alisema: “Siwezi kuongea mengi, lakini nataka kuwahakikishia Watanzania na mashabiki wangu kuwa nitalinda rekodi yangu ya kutopoteza mchezo kwenye ardhi ya nyumbani hivyo ni lazima Mthailand akae.”

Naye Mancito alijibu kwa kusema: “Nimewahi kuwapiga mabondia wagumu kutoka Amerika na hata Mexico, hivyo naamini Mtango hawezi kufika raundi ya pili.”

Mbali ya mapambano hayo usiku huo kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi yatakayokuwa kati ya Adam Chiga dhidi ya Adam Kipenga, Ramadhani Shauri dhidi ya Salehe Mkalekwa, Japhet Kaseba vs Iman Mapambano, Selemani Kidunda kutoka JWTZ atazichapa na Said Mbelwa, na Ismail Caliatano pia wa JWTZ akizipiga na Mustafa Doto. Kwa upande wa kina dada, Stumai Muki atamalizana na Lulu Kayage.

Tiketi za pambano hilo zinauzwa kwa Sh 20,000 mzunguko, Sh 5,000 kawaida na Sh 100,000 kwa VIP zikipatikana kupitia Nilipe App, maduka ya Vunja Bei Store na Vunja Bei Toto Sinza, Shishi Food (Kinondoni), pia Cake City ya Salasala. Sehemu nyingine ambazo tiketi zitakuwa ni Kaites Lounge ambayo inapatikana Tabata na Dickson Sound ya Magomeni.

Joel Thomas na Careen Oscar


Toa comment