Pierre Alivyonusurika Kifo Cha Corona

DAR: MCHEKESHAJI kwenye mitandao ya kijamii Bongo, John Mollel ‘Pierre Liquid’ amesimulia jinsi alivyonusurika kifo baada ya kushambuliwa na Ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na Virusi vya Corona.

 

Wiki tatu zilizopita, Pierre alikuwa kwenye hali mbaya baada ya kupata Corona ambapo mwenyewe anakiri kuchungulia kaburi kabla ya Mungu kumnusuru.

 

Katika mahojiano maalum (exclusive) na Gazeti la IJUMAA baada ya kuruhusiwa kutoka karantini, Pierre anasema, ugonjwa huo umempa somo kubwa na kuwa na sababu ya kutulia nyumbani na kuacha kuzurura sehemu ambayo haina ulazima wa kwenda, kwani yeye yamemkuta.

 

IJUMAA: Pole sana kwa kuumwa Corona. Je, uliupatia wapi ugonjwa huo au ulisafiri?

Pierre: Asante sana. Sikusafiri popote, nafikiri nilipata kwenye mikusanyiko ya watu, tena ile ya kukutana kwenye pombe.

 

IJUMAA: Ulianza kujisikiaje hadi ukagundua inaweza kuwa ni Corona?

Pierre: Siku hiyo niliamka asubuhi, nikajikuta nasikia mwili wote unauma, kifua kinabana, kichwa ndiyo usiseme kabisa. Ilibidi niende Hospitali ya Temeke (Dar). Hapo nililazwa na kuchukuliwa vipimo, ndipo wakagundua nina Corona.

 

IJUMAA: Ulipokeaje majibu kwamba una Corona?

Pierre: Baada ya kuambiwa nina Corona, kwa kweli nilishtuka, lakini nikajipa moyo kwamba ugonjwa huu ni wa dunia nzima. Hivyo, nikajipa moyo tu na kuanza kukaa karantini kwenye Hospitali ya Amana (Ilala).

 

IJUMAA: Kuna video ilisambaa mkifanya birthday mkiwa karantini pale hospitalini. Je, ilikuwaje?

Pierre: Siku hiyo ilikuwa kama kesho yake tunatoka kwa sababu sisi tulikuwa tuna afadhali, maana huwezi ukang’ang’ania kukaa hospitalini huku kuna wengine wako kwenye hali mbaya zaidi.

 

IJUMAA: Sasa hivi unajisikiaje na umeshapima tena na kuambiwa virusi vimeisha kabisa?

Pierre: Kwanza mimi tangu nilivyotoka karantini, niliambiwa nisitoke ndani hadi tarehe 30 (jana), nafikiri na muda huo watakuwa wamenipa majibu ya maendeleo ya afya yangu.

 

IJUMAA: Sasa hivi nani anakuhudumia?

Pierre: Ni mimi mwenyewe, inabidi niwe peke yangu.

IJUMAA: Unawashauri nini watu wengine ambao wamegundulika kuwa na Virusi vya Corona na kuwa na hofu?

 

Pierre: Kwanza waondoe hofu, maana hofu ndiyo ugonjwa wenyewe wala siyo Corona, kisha wafuate tu maelekezo ya wataalam kama nilivyofanya hadi nikanusurika.

Mbali na Pierre, watu wengine maarufu Bongo walioripotiwa kupata Corona na kupona, ni pamoja na MwanaFA na mmoja wa mameneja wa Wasafi, Sallam Sk.

Stori: IMELDA MTEMA, Ijumaa


Loading...

Toa comment