PIERRE ASIPOFUNGA ZIPU …? APEWA TAHADHARI

ASIPOFUNGA zipu yatamkuta! Ndiyo mijadala inayoendelea katika mitandao ya kijamii baada ya picha mbalimbali kusambaa zikimuonesha jamaa aliyejizolea umaarufu Bongo kwa staili yake ya kuchapa ‘maji’, Peter Mollel ‘Pierre’ akiwa na mastaa tofauti wa filamu na muziki. 

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafuatiliaji wa mambo ya kiburudani katika mitandao walitoa mitazamo yao chanya kuwa, Pierre ambaye hupenda pia kutambulika kama Konki Liquid apunguze kuwa karibu na warembo kwani mwisho wake huwa si mzuri.

 

“Namsihi sana, najua ustaa ni mzigo na mara nyingi huwatesa wengi wanapokuwa maarufu hivyo nimsihi sana Pierre kwa hizi picha zinazosambaa mitandaoni  mara leo yupo na staa flani tena katika mapozi ya kimahaba kwani mwisho wake atajikuta ameshazama penzini,” alisema Almasi Joseph mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar.

Alfred John kutoka Kimara Baruti jijini Dar anasema kuwa, Pierre anapaswa kufungwa zipu mapema iwezekanavyo kwani anaweza kujikuta akaanzisha uhusiano ambao sio. “Jamaa nimemfuatilia sana na nakumbuka mara ya mwisho alisema kuwa hana mchumba kwa hiyo mastaa hata wanawake wengine wataingia kwa gia ya kuwa naye na mwisho wa siku wakampa magonjwa ya ajabu.”

 

Dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Beatrice naye alichangia kwa mtazamo wa kumuona Pierre anachofanya ni sawa lakini achague marafiki wa kuwa nao. “Mimi kwa mtazamo wangu naona Pierre ni sawa kupiga picha na mastaa tena kwa mahaba hao wenye wivu wajinyonge wenyewe jamani. Ila anachotakiwa ajichunge kidogo kuna marafiki mastaa wengine siyo kabisaaa,” alisema Beatrice.

Picha mmojawapo inamuonesha msanii wa filamu Bongo, Wema Sepetu akiwa na Pierre ambapo picha hiyo ilipigwa siku alipotembelewa nyumbani kwake na baada ya kufika alionekana kuchangamka kwa kuwasalimia watu kisha akakumbatiana na Wema kimahaba kama mtu na mpenzi wake.

 

Pia katika picha nyingine Pierre anaonekana akiwa na muuza nyago kwenye video za Kibongo, Sasha Kassimu ambapo napo inaelezwa siku iliyopigwa alikuwa amekwenda kusaini dili la ubalozi. Mbali na Wema na Sasha, kuna picha nyingine zinamuonesha Pierre kwa nyakati tofauti akiwa na wauza nyago kwenye video za Kibongo, Tunda na Amber Lulu ambao wamemkumbatia kimahaba.

Licha ya Pierre kutokea kujizolea umaarufu kupitia staili yake ya kunywa maji huku akitamka maneno ya kuchekesha kama; mama nakufaa! Ametokea kujipatia madili mengi ya kuwa balozi kwenye makampuni mbalimbali sambamba na kupata shoo ndani na nje ya nchi kwenda kujumuika na watu na kuwachekesha.

 

Ameshapata shavu Kenya na kwa sasa yupo nchini Marekani alipoalikwa kwenye shoo nyingine. Pia amepata mualiko kutoka kwa mchezaji wa Timu ya Tottenham ya nchini Uingereza ambaye ana asili ya Kenya, Victor Wanyama kwenda nchini Uingereza akiwa na staa wa Muziki wa Bongo Fleva. Omari Nyembo ‘Ommy Dimpoz’.

Toa comment