The House of Favourite Newspapers

Piga,ua utapitia haya penzini, jifunze!

YAWEZEKANA unapokuwa kwenye eneo salama katika uhusiano, unaweza usifikirie wale wanaopitia magumu, lakini nikuambie tu, uhusiano una nyakati tofautitofauti hivyo ni vyema kujifunza.  Ndugu zangu, kwenye mapenzi kuna milima na mabonde kama vile yalivyo maisha ya kawaida. Kuna wakati unaweza kufurahi sana, kuna wakati unaweza kuhuzunika sana.

Ndiyo maana leo nimekuja na mada hii kama inavyojieleza hapo juu. Nitazungumzia mambo ambayo unaweza kukutana nayo kama utaingia kwenye penzi bila kujali umri, elimu, uwezo, rangi, kabila wala wadhifa ulionao lazima tu kuna mambo au mapito ambayo utayapitia, iwe kwa kutaka au kwa kutotaka.

Ingawa mapito ya mambo haya yanatofautiana kutoka kwa mtu mmoja na mwingine, lakini kwa jumla wake ni lazima tuyapitie hivyo karibu ujifunze;

FURAHA

Mara nyingi mwanzoni mwa mapenzi kwa sababu penzi lenu ni jipya, unaweza kupitia furaha na vicheko vya hapa na pale kwa sababu bado penzi lenu ni jipya linalowafukuta mioyoni mwenu. Kila mtu anampenda na ana hamu na mwenzake.

Usibweteke na hilo, kuna wakati mambo yanaweza kuwa tofauti hivyo jiandae pia. Ikitokea furaha imeondoka, wenye jukumu la kuirudisha ni ninyi wapendanao.

HUZUNI

Lakini lazima ujue kuwa furaha pacha wake huwa ni huzuni hivyo kuna kipindi cha huzuni unapaswa kukipita au utakuja kukipita kwa namna yoyote ile na ndiyo maana hata mnapofungishwa ndoa huwa mnaulizwa kuwa mko tayari kuishi na kusaidiana kwenye shida na raha?

MATESO

Ukiwa kwenye penzi, kuna wakati unaweza kuingia kwenye mateso juu ya mpenzi wako, aidha, mateso ya hisia, maneno au matendo ambayo yanaweza kukukwaza na kukutesa kila anapoyafanya au unapoyafikiria.

MACHOZI

Kuna wakati kutokana na makwazo na mateso ambayo unayapata kwa mwenza wako, moyo huzalisha huzuni ambayo mwisho wa siku husababisha kulia kwa uchungu, kwa sababu nafsi yake haitaki kuamini kama matendo na maumivu unayoyapata yanasababishwa na mwenza wako ambaye mlianza naye kwa furaha.

UTAKATA TAMAA

Kutokana na changamoto ambazo unakutana nazo kwenye uhusiano wako, kuna wakati unaweza kufikia hatua ya kukata tamaa ya kuendelea kuishi na mpenzi, mchumba au mumeo kwa kudhani labda ulikosea kumchangua.

UAMUZI MBAYA

Kwa makwazo ambayo unaweza kuyapata au umeyapata kwa umpendaye, mtima wako umekuwa na maumivu ya mara kwa mara na unaweza kufikia au kuchukua uamuzi mbaya na hatari kama kumzuru kwa kumuwekea sumu, kumchinja, kumpiga, kumwagia mafuta, maji ya moto na mawazo mengine mabaya kama hayo. Ndiyo

maana umekuwa ukisikia, kuona au kusoma matukio mabaya na ya kinyama yakifanyika kwenye jamii yetu.

Ndugu yangu, usiyape nafasi mawazo hayo mabaya ambayo yanaweza kugharimu maisha yako kwa kukupeleka jela au kupoteza uhai wako.

Unapopatwa na mawazo mabaya juu ya mwenza wako ni vyema ukaepuka kutoa adhabu au kufikiria mabaya kwa kukaa naye mbali kwa muda ili hasira zikuishe ndipo umsogelee.

Unaweza kunifuata kwenye kurasa za mitandao ya kijamii; Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

Comments are closed.