Pikipiki ya 4 Yakabidhiwa, Mume, Mke Wageuka Kivutio Tusua Maisha na Global
Hatimaye washindi wa droo ya nne ya tusua maisha na Global, wamekabidhiwa zawadi zao Ijumaa katika Ofisi za Global Publishers, Sinza Mori jijini Dar es Salaam ambapo wanandoa Asha Kombo na mumewe, Omary Kisigalile wamegeuka kivutio wakati wakikabidhiwa zawadi.
Asha aliyebuka mshindi wa ada ya shule katika droo iliyochezeshwa mubashara kupitia Global TV Online, amefika katika ofisi za Global akiwa ameambatana na mumewe na alipopewa nafasi ya kuzungumza chochote baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, alianza kwa kumshukuru mumewe kwa jinsi anavyomjali, kiasi cha kuacha kazi zake zote na kumsindikiza kupokea zawadi.
“Mume wangu ameniwekea bili ya magazeti, mimi kila siku naletewa magazeti mpaka mlangoni na gazeti ninalolipenda zaidi niIjumaa, yeye huwa anasoma Championi, kwa hiyo hata huu ushindi wa leo, ni kwa ajili yake,” alisema Asha na kuongeza kwamba ada aliyoshinda, atamlipia mwanaye anayesoma kidato cha kwanza na kumnunuliamahitaji, lakini pia atamlipia mwanaye mwingine anayesoma shule ya kulipia.
“Unajua siku hizi sawa wanasema elimu bure lakini kuna mahitaji muhimu ambayo ni lazima uwe na fedha, nawashukuru sana Global kwa hiki mlichokifanya, Mungu awabariki sana.
Naye Abbas Shekwavi ambaye amemwakilisha mshindi wa pikipiki, Hassan Shekwavi kutoka Dodoma, amesema awali alikuwa haamini kama ni kweli mtu yeyote anaweza kuwa mshindi lakini baada ya kushuhudia kaka yake akiibuka na pikipiki mpya, atakuwa balozi mzuri wa kuwaelimisha wengine.
“Ndugu yangu ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Tambukareli, Dodoma na hana mtu yeyote anayefahamiananaye hapa Global, niliposikia ameshinda na leo nakabidhiwa zawadi kwa niaba yake, kwa kweli nimefarijika sana ndani ya moyo wangu na namuomba Mungu awabariki viongozi na wafanyakazi wote wa Global. Kazi mnayoifanya ni kubwa sana.
Mwingine ambaye alipaswa kukabidhiwa zawadi yake leo, ni Mary Mwalingo wa Mbeya ambaye hakuwa na mwakilishi hapa jijini Dar es Salaam, hivyo ameshindwa kuhudhuria zoezi la kupokea zawadi lakini atatumiwa zawadi yake ya dinner set na kukabidhiwa na wakala wetu mkoani Mbeya.
Comments are closed.