The House of Favourite Newspapers

Pluijm amrejesha Busungu kikosi cha kwanza

0

pluijm1Sweetbert Lukonge Dar es Salaam

KOCHA Mkuu ya Yanga raia wa Uholanzi, Hans van Der Pluijm, ameamua kumrejesha katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, mshambuliaji Malimi Busungu aliyekuwa akisugua benchi tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Pulijm amefikia hatua hiyo baada ya kuamini kile alichoambiwa na Busungu siku chache kabla ya mechi ya juzi Jumamosi ya Simba na Yanga wakati kikosi cha timu hiyo kilipokuwa kisiwani Pemba kikijiandaa.

Inadaiwa kuwa Busungu alimvaa kocha wake huyo na kumtaka ampatie japo dakika 30 za kucheza katika mechi hiyo ili aweze kuwatungua Simba lakini Pluijm hakutilia maanani ombi lake hilo.

Hata hivyo, kushindwa kufanya vizuri kwa Simon Msuva katika dakika za kwanza za mchezo huo, kulimfanya Pluijm amtoe na kumuingiza Busungu ambaye kuingia kwake kuliifanya Yanga kuongeza mashambulizi langoni mwa Simba.

Katika dakika ya 80, Busungu alifanikiwa kuifungia Yanga bao la pili na kujikuta akimpagawisha vilivyo Pluijm lakini pia akimwacha na maswali mengi kuhusiana na ombi lake alilomwomba la kumpatia dakika 30 za kucheza kwenye mchezo huo wakati walipokuwa wamepiga kambi Pemba.

Hata hivyo, jana Jumapili, Busungu ameliambia Championi Jumatatu: “Baada ya mechi nilikutana na kocha na amenihakikishia kuwa sasa atakuwa akinipatia muda wa kutosha uwanjani na ikiwezekana nitakuwa nikianza katika kikosi cha kwanza.

“Amefanya hivyo baada ya kuamini kile nilichomwomba wakati tulipokuwa Pemba, kuwa anipatie dakika 30 za kucheza ili niweze kuifunga Simba, jambo ambalo nimelifanya,” alisema Busungu ambaye, pia amemwagiwa sifa nyingi na Pluijm

akisema kuwa anafurahishwa na aina ya uchezaji wake na ana njaa ya mabao.

Leave A Reply