The House of Favourite Newspapers

Pluijm ashtukia, achimba mkwara Ligi Kuu Bara

0

pluijm (1)

Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm

Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
HUKU timu yake ikijitupa uwanjani leo Jumatano kucheza na Toto Africans ya Mwanza, Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ametamka kuwa hataidharau timu yoyote atakayovaana nayo kwenye Ligi Kuu Bara.

Kauli hiyo ameitoa siku moja kabla ya mechi hiyo ambayo itapigwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Yanga kwenye mchezo uliopita dhidi ya Azam FC, ilitoka sare ya kufungana bao 1-1, huku mchezo huo ukiwa umejaa upinzani mkubwa.

Akizungumza na Championi Jumatano, Pluijm alisema kikubwa alichokigundua ni kila timu kucheza kwa kupania inapokutana na Yanga kwa lengo la kutaka kuwafunga.

Pluijm alisema hali hiyo alianza kuiona kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo waliingia uwanjani kwa kupania, lakini wakawafunga mabao 2-0, yaliyofungwa na Donald Ngoma na Malimi Busungu.

“Nimejifunza vitu vingi ndani ya muda mchache tangu ligi kuu imeanza, ukiangalia mechi ambazo tumezicheza, kila timu tutakayocheza nayo inaingia uwanjani kucheza na sisi kwa kutupania.

“Hiyo yote ni kutaka kutuvuruga na kusababisha mpira uwe mgumu kwa wachezaji wangu, kunakuwa na rafu za mara kwa mara, kitu ambacho siyo sahihi.

“Hivyo katika mechi hivi sasa nitaingia kwa tahadhari kubwa ya kila timu kutupania, hivyo nitakachokifanya ni kukiandaa kikosi changu kabla ya mechi ili mwisho wa mechi tuibuke na ushindi na hilo linawezekana kutokana na ubora wa kikosi changu,” alisema Pluijm.

Leave A Reply