The House of Favourite Newspapers

Pluijm: Azam FC wanakufa mapema

0

pluijm

Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.

Wilbert Molandi,
Dar es Salaam
KATIKA kuhakikisha anapunguza presha ya mechi dhidi ya Azam FC, Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ameendelea kukiimarisha kikosi chake kwa kuwapa mbinu mbalimbali zitakazowapa ushindi wa mapema kwenye mchezo huo.

Timu hiyo, imeweka kambi yake katika Hoteli ya Landmark, jijini Dar es Salaam huku ikiendelea kujifua kwenye Uwanja wa Boko Veterani.

Yanga na Azam FC zinatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar kuvaana katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa Jumamosi hii.

Kocha huyo, katika mazoezi ya juzi Jumatatu, alionekana akiwataka wachezaji wake kucheza soka la kasi huku wakishambulia muda mwingi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Pluijm alisema kikubwa anawapa mafunzo wachezaji wake ya kucheza soka la pasi za haraka wakati wanashambulia lango la timu pinzani ili apate ushindi wa mapema.

“Kama unavyojua hivi sasa nipo kwenye maandalizi ya mechi dhidi ya Azam, hivyo ninaendelea kuziboresha baadhi ya nafasi, ikiwemo ya ushambuliaji ili kuhakikisha ninapata ushindi wa mapema kwa ajili ya kupunguza presha ya mechi.

“Yanga hivi sasa inapaniwa sana, hiyo ni kutokana na kila timu kutaka kutufunga, hivyo hali hiyo inasababisha presha ya mechi kuwa kubwa ndani ya uwanja.

“Ili presha ya mechi ipungue, basi nipate ushindi wa mapema ili wachezaji wangu wacheze kwa kujiamini na hilo linawezekana kutokana na maandalizi ninayoyafanya,” alisema Pluijm.

Leave A Reply