Pluijm eti anataka soka la Wenger Yanga

wengerArsene Wenger

Na Sweetbert Lukonge

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amekubali yaishe kwa kusema sasa anataka mabao tu na haina haja kupiga pasi nyingi wakati timu inataka ushindi, naye Hans van Der Pluijm wa Yanga ameiga.

Wakati Wenger akitamka maneno hayo katikati ya wiki hii, Pluijm raia wa Uholanzi anayeinoa Yanga amesema maneno hayo jana Ijumaa wakati timu yake ilipofanya mazoezi ya mwisho kabla ya leo kuivaa Mbeya City.

pluijm1.jpgHans van Der Pluijm wa Yanga.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Pluijm alisema kuwa kuanzia sasa kikosi chake kitakuwa kikicheza soka la kasi na lisilokuwa na pasi nyingi, falsafa ambayo Mfaransa Wenger anaitumia sasa Arsenal.

Pluijm alisema sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kuhakikisha anapata matokeo mazuri katika mechi zake zote zilizobakia katika ligi kuu hiyo inayoshirikisha timu 16.

“Tunakabiliwa na changamoto nyingi katika kutetea ubingwa wetu hivyo tunatakiwa kuwa makini zaidi ili kuhakikisha tunatimiza lengo letu hilo.

“Kwa sasa nimelazimika kubadili aina ya uchezaji wa kikosi changu kwani hatutacheza tena kama zamani ambapo tulikuwa tunapiga pasi nyingi na kutengeza nafasi za kufunga kama wengine wanavyopenda.

“Pasi nyingi pasipo matokeo mazuri si lolote, siku zote muhimu ni kutumbukiza mpira wavuni na siyo mambo mengine,” alisema Pluijm.


Loading...

Toa comment