The House of Favourite Newspapers

PM Majaliwa: Huduma Jumuishi za Kifedha ni Kiungo Muhimu Cha Ukuaji Uchumi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw Kassim Majaliwa amezindua rasmi huduma za kidijitali za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) inayofahamika kama ‘NBC Kiganjani’ huku akitoa wito kwa mashirika na taasisi za fedha nchini kuhakikisha zinaboresha mifumo ya huduma za kielectronic kwa kuoanisha mifumo baina ya taasisi hizo.
Alisema hatua hiyo itarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi zikiwemo utunzaji, utumaji na upokeaji wa fedha (Financial Inclusion).

Waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kusimamia uhamasishaji wa matumizi ya mfumo wa malipo kwa njia za kidigitali katika utoaji wa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo matumizi ya mashine ya POS na kadi hatua ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuchochea biashara ya ndani kwa kuwezesha miamala ya malipo kufanyika kwa uharaka, salama, na unafuu.

Hafla uzinduzi huo imefanyika leo jijini Dar es Salaam ikihudhiriwa pia na Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba (Mb), Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw Saad Mtambule na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bi. Sauda Msemo.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC Bw Theobald Sabi, aliwaongoza wafanyakazi wa benki hiyo sambamba na wadau mbalimbali wa sekta ya michezo walioongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Bw Wallace Karia.

“Ni kutokana na kutambua umuhimu wa huduma za kidigitali katika utoaji wa huduma za kifedha katika kuchochea ukuaji wa uchumi ndio sababu Rais Samia Suluhu Hassan amenitumia nije kuwapongeza benki ya NBC kwa hatua hii muhimu ya mapinduzi ya kidigitali katika utoaji wa huduma za kifedha nchini…hongereni sana,’’ alipongeza
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, hatua ya benki hiyo itasaidia serikali kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa njia za kidijitali, kupunguza mianya ya ukwepaji wa kodi, na kuongeza uwazi katika mifumo ya fedha.
Naye Bi Msemo pamoja na kupongeza hatua hiyo ya NBC, alitoa rai kwa taasisi za fedha nchini kuhakikisha zinawekeza zaidi kwenye mifumo ya kiulinzi kwa njia za kidigitali ili kuhakikisha usalama wa fedha za wateja wao kwa kuwa ukuaji unaoshuhidiwa sasa wa huduma za kidigitali unakwenda sambamba na ongezeko la wizi wa kupitia njia za kidigitali.

Awali akizingumza kwenye hafla hiyo Bw Sabi alisema huduma hiyo iliyoboreshwa ya Aplikesheni ya NBC Kiganjani na huduma ya NBC Lipa Kiganjani(Lipa namba ya NBC), zinalenga kuleta mapinduzi ya mfumo wa fedha nchini kwa manufaa ya Watanzania wote.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw Kassim Majaliwa (katikati) akiongoza zoezi la uzinduzi rasmi huduma ya kidijitali za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) inayofahamika kama ‘NBC Kiganjani’
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw Kassim Majaliwa (pichani) akizungumza kwenye hafla hiyo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw Kassim Majaliwa (katikati) akifurahia jambo sambamba na Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba (Mb) (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji Bw Theobald Sabi (kulia) wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa huduma ya kidijitali za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) inayofahamika kama ‘NBC Kiganjani’ wakati iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam


Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bi. Sauda Msemo (pichani) akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Biashara Bw Elvis Ndunguru (kushoto) akiongoza mjadala wakati wa hafla hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya NBC na wageni waalikiwa wakifuatilia uzinduzi huo.