Pointi 3 za Simba Kimenuka!

Beki wa Kagera Sugar, Mohamed Fakhi.

Sweetbert Lukonge | Championi Ijumaa | Habari

SAKATA la beki wa Kagera Sugar, Mohamed Fakhi kudaiwa kucheza akiwa na kadi tatu za njano limechukua sura mpya na pointi tatu ambazo wamepewa Simba kutokana na tukio hilo, zimefika kwenye hatua mbaya.

Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara.

Simba ilipoteza mchezo wao dhidi ya Kagera kwa mabao 2-1 lakini baada ya kukata rufaa, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kupitia Kamati ya Saa 72, likaipa Simba ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kwa kile kilichoonekana Kagera walikiuka kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Lakini baada ya Kagera kuomba kupitiwa upya kwa hukumu hiyo ikidai Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano ndipo mambo yamezidi kuwa makubwa.

Kikosi cha timu ya Simba.

SIMBA KUPOKWA POINTI 3

TFF kupitia Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ilipokutana Jumanne ya wiki hii kupitia hukumu iliyoipa Simba pointi tatu huku wadau wengi wakihojiwa, ikashindikana kutolewa maamuzi ya mwisho.

Taarifa ambazo hazikuwa rasmi hadi jana jioni ilidaiwa kuwa kamati hiyo ilikuwa na mpango wa kurejesha pointi tatu kwa Kagera kwa kuwa hukumu ilifanyika kimakosa.

Wachezaji wa timu ya Kagera.

“Kamati ilikutana jana (juzi Jumatano) katika sehemu ambayo hakuna mwandishi yeyote aliyeruhusiwa kuwepo wala hawakupajua, waliamua iwe hivyo ili kukwepa usumbufu wakihisi waandishi wanaweza kuvuruga kazi yao,” alisema mtoa taarifa kutoka katika moja ya kamati zilizohusika na mchakato huo, kisha akaendelea:

“Kikao chao kilimalizika na wameshachukua maamuzi lakini bado hawajakabidhi ripoti, sijajua kuna nini wanachosubiri lakini walikamilisha ileile jana (juzi) usiku na hivi ninavyoongea na wewe tayari wameshakamilisha kazi yao.”

HOFU YATANDA MSIMBAZI

Kigogo mmoja wa Simba alipozungumza na gazeti hili aliweka wazi kuwa ana hofu TFF watarejesha pointi kwa Kagera wakati wao wanaamini suala lipo wazi kuwa Kagera walifanya makosa.

YANGA IMESHIKA MPINI

Mtoa taarifa mwingine ambaye ni mkongwe kwenye mambo ya soka na amekuwa akifanya kazi kwa ukaribu na TFF na kamati zake, alisema haya:

“Unajua Yanga walipata taarifa mapema kuwa kuna dalili za mchezo mchafu unaotaka kufanyika, sasa wakawahi kuchukua taarifa za waamuzi kuhusu mchezo huo, walifanya hivyo ili kama kuna mabadiliko yoyote ambayo yanataka kufanywa wao wawaumbue.

Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Salum Mkemi.

“Hilo limewatisha hao wanaotaka kutoa maamuzi na ndiyo maana ukaona wanajiumauma kutoa maamuzi, wewe hujiulizi hilo jambo ni dogo la kuchukua ripoti tu ya mwamuzi na kamisaa wa mchezo unaolalamikiwa lakini wao wakawahoji watu wengi!”

SIMBA YANUSA HARUFU, YAKINUKISHA

Inaelezwa kuwa mabosi wa Simba walishtukia kuwa kuna dalili za wao kupokwa pointi zao hizo za mezani na ndiyo maana juzi kupitia ofisa wao habari, Haji Manara walitoa tamko kali kuhusu Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuwa anatakiwa kujiuzulu kwa kuwa ameshindwa kusimamia vizuri maendeleo ya soka nchini.

Manara alisema Malinzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Soka wa Mkoa wa Kagera, hatendi haki kwa Simba na amefanya hivyo zaidi ya mara moja akitoa mifano ya matukio kadhaa.

YANGA YAMALIZA MCHEZO, YAJITOA

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga na ambaye ndiye alikuwa msemaji mkuu wa klabu hiyo kulipinga suala hilo, Salum Mkemi alisema:

“Sisi tumeamua kukaa kimya kwanza ili tuiache kamati hiyo ya TFF imalize kazi yake kwa umakini zaidi. Baada ya kusikia maamuzi yao ndipo tutatoa hukumu.”

SIMBA YAIVAA YANGA

Aidha, Manara aliijia juu Yanga kwa jinsi ambavyo imekuwa ikilizungumzia suala hilo la Fakhi kwa kusema haliwahusu lakini wamekuwa mstari wa mbele kudili nalo.

“Tunashangazwa na Yanga wanavyodili na mambo yetu na kuacha kufanya yao jambo ambalo liliwasababisha watolewe kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na MC Alger kwa sababu tu wanang’ang’ania vitu ambavyo haviwahusu.

“Hili suala letu la kupewa pointi linatuhusu sisi na watu wa kamati hata kama tumepewa au tutapewa pointi za mezani wao haliwahusu hata kidogo na wasijiingize ndani yake kwani wao siyo wahusika,” alisema Manara.

MBIO ZA UBINGWA ZIMEKOLEA

Simba ipo kileleni katika ligi kuu ikiwa na pointi 62, kama haitapokwa pointi hizo tatu, kisha ikashinda michezo mitatu iliyosalia itafikisha pointi 71, Yanga ina pointi 56, ikishinda mechi tano zilizosalia itafikisha pointi 71 pia.

Ikiwa itakuwa hivyo Yanga inaweza kuwa na nafasi kubwa ya ubingwa kwa kuwa ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Ikiwa Simba itapokwa pointi, itabaki na pointi 59 na ikishinda michezo yote itafikisha pointi 68 wakati Yanga ikishinda zote itafikisha 71 na hivyo kuwa mabingwa.

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment