The House of Favourite Newspapers

Pointi 3 za Ubingwa Yanga Hizi Hapa

0

NA WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA | CHAMPIONI JUMAMOSI | DAR ES SALAAM

YANGA ina mambo matatu ambayo inaamini yataipa ubingwa kwa kuwawezesha kushinda mechi zote tano za Ligi Kuu Bara walizobaki nazo hadi sasa. Ipo hivi, licha ya Simba kutishia kwenda Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kudai pointi walizopokwa baada ya kupewa awali, Yanga wenyewe wameweka malengo ya kuhakikisha wanashinda michezo yote iliyobaki.

Hadi mazoezi ya jana asubuhi yanamalizika, wachezaji wa Yanga walikuwa na jeuri ya kutwaa ubingwa kutokana na pointi au hoja tatu;

MASHABIKI WAO

Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima aliliambia Championi Jumamosi kuwa, mashabiki wa Yanga wanatakiwa kujitokeza kwa wingi uwanjani katika mechi zao hasa zile za Dar es Salaam ili kuzizima kelele za mashabiki wa Simba wanaowazomea kila mara. “Mashabiki wetu wakijaa, zile kelele za Simba hazitopata nguvu na Yanga tutatawala uwanja mzima hii ni silaha kubwa kwetu ya ushindi, naomba mashabiki waje kwa wingi,” alisema Niyonzima.

KUREJEA KWA BOSSOU, YONDANI

Faraja na silaha nyingine ya Yanga ni kurejea kikosini kwa mabeki wa kati Kelvin Yondani na Vincent Bossou ambao walikuwa majeruhi. Yondani alikuwa akiumwa Malaria na Bossou yeye alikuwa anasumbuliwa na goti, hivyo uwepo wao leo utaziba pengo la Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye hatakuwepo kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

POSHO YA LAKI MBILI

Kuanzia mechi ya leo dhidi ya Prisons, wachezaji wa Yanga watakuwa wakipata posho ya Sh 200,000 na kwa kuanzia jana walipewa kabla hata ya kucheza mechi ya leo. “Tumepewa fedha hizi kama posho kuelekea mechi yetu na Prisons, ni motisha ili tushinde na tutashinda, hatuna uhakika ila tumeambiwa mambo yatakuwa hivi katika mechi zetu zilizobaki,” alisema mmoja wa wachezaji wa Yanga.

WAPO VIZURI

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi akizungumzia mchezo wa leo, alisema: “Kikosi chetu kimejiandaa vizuri na tuna mbinu kadhaa za ushindi, Prisons ni timu nzuri ila sisi tunataka pointi tatu tujiweke mahali kuzuri tutwae ubingwa.”

Naye Niyonzima alisema: “Naomba mashabiki wa Yanga waje kwa wingi kutushangilia, sisi tupo vizuri kushinda mechi hii.”

Kocha wa Prisons, Abdallah Mohamed, akizungumzia mechi hiyo, alisema: “Tumejiandaa kushinda mechi hii na hatutakubali kufungwa tena na Yanga kwani walitufunga katika robo fainali ya Kombe la FA hapahapa Dar es Salaam, hatukubali.”

Leave A Reply