POLISI ALIYEKUTWA AMEKUFA CHUMBANI…SIMANZI

KIFO cha polisi wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU), Justine Alfred Marobo kimeacha simanzi nzito kufuatia askari huyo kuwa kipenzi cha watu huku mazingira ya kifo chake yakishindwa kufahamika vizuri.  

 

Alfred alikutwa na umauti Januari 26, mwaka huu katika kota za polisi, Mabatini jijini Mwanza alipokuwa anaishi na mke pamoja na mkwewe. Mmoja wa wanafamilia ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini, alilieleza Risasi Jumamosi kuwa, kama ndugu wameshindwa kufahamu moja kwa moja mazingira ya kifo cha ndugu yao kwani kwenye tukio hilo yamezungumzwa mengi.

 

“Unajua tumeshindwa kufahamu nini hasa kimemsababishia mauti maana ndugu yetu alikuwa mzima tu wa afya lakini ghafla tukaambiwa amekutwa amekufa chumbani kwake, wengine wanasema amekutwa sebuleni amekufa kwa hiyo tunashindwa kuelewa ukweli ukoje,” alisema ndugu huyo.

 

Hata hivyo, ndugu huyo alieleza kuwa, anashukuru Jeshi la Polisi limechukulia kwa uzito suala hilo na kutokana na mazingira tata ya kifo cha Alfred tayari kuna watu kadhaa wanawashikilia kwa ajili ya uchunguzi kwani wanashukiwa kuhusika na tukio hilo. “Watu wengi tunasubiri kwa hamu ripoti ya polisi kuhusu kifo cha ndugu yetu huyu maana tunaamini ndiyo wataeleza ukweli,” alisema.

Baadhi ya askari ambao walikuwa wakiishi jirani na marehemu Alfred walisema wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo hicho na kwamba wanaamini kuna kitu nyuma ya pazia kilichosababisha tukio hilo hivyo wanaachia polisi wafanye uchunguzi wao. “Ni simanzi kubwa. Kifo cha Alfred kimetuachia huzuni kubwa, ni mtu ambaye alikuwa akiishi vizuri na kila mtu, tutamkumbuka daima,” alisikika mmoja wa askari hao wakati wa kuaga mwili wa marehemu jijini Mwanza.

 

Mwili wa Alfred uliagwa Jamanne iliyopita jijini Mwanza ambapo maofisa mbalimbali wa polisi walimuaga akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna. Mara baada ya mwili huo kuagwa na ndugu jamaa na marafiki wa jijini Mwanza, ulisafirishwa hadi nyumbani kwao Kijiji cha Mowo Njamu, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.

 

Ibada ya mazishi ilifanyika Jumatano iliyopita, nyumbani kwa marehemu ambapo mahubiri yalitolewa na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Siha Sango, Cathubet Temba ambaye katika mahubiri yake alihubiri kuhusu upendo.

Alisema ni vyema watu wakapendana, mume akampenda mke na mume akampenda mke. Hata hivyo, Risasi Jumamosi lilishindwa kupata maelezo ya ndugu wa Alfred kwa kile kilichoelezwa kuwa wameliachia jeshi la polisi lifanye uchunguzi wake. Marehemu Alfred aliyeacha mke na watoto watatu, alizikwa katika Makaburi ya Kijiji cha Mowo Njamu ambapo yalihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.

 

Juzi, Risasi Jumamosi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna ili kujua undani wa kifo hicho ambapo alipopatikana alisema yupo nje ya ofisi, akaomba atafutwe kaimu wake ambaye ni Advera Bulimba.

Alipotafutwa Bulimba, alisema suala hilo bado lipo kwenye uchunguzi hivyo hawezi kulizungumzia sana kwani anaweza kuharibu uchunguzi. Alipoulizwa kuhusu idadi ya watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo, Kamanda Bulimba alisema pia hawezi kutaja kwa kuwa bado wapo kwenye uchunguzi.

STORI: Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Toa comment