The House of Favourite Newspapers
gunners X

Polisi Anaswa Kujiunganishia Umeme, Akutwa na Viroba…

0

 

MKUU wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi, amemkamata polisi ambaye alikuwa akiiba umeme wa TANESCO ambao alijiunganishia kinyume na sheria na kuweka swichi chooni ambayo ndiyo ilikuwa inatumika kuiba umeme huo na kukwepa kulipa bili ya umeme hivyo kuiingizia hasa serikali.

 

Kihongosi amesema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo walimpekua katika nyumba yake anayoishi pamoja na gari yake binafsi na kumkuta na maboksi ya viroba vya Konyagi ambavyo vilipigwa marufuku na serikali miaka kadhaa iliyopita.

 

Imeelezwa kuwa, askari huyo amekuwa akivitumia kwa kujaza katika chupa za konyagi na kuziuza kwa wananchi katika baa yake, pia wamekamata kete 20 za bangi ambazo alizihifadhi vizuri katika pochi maalumu na kuzificha katika gari yake.

 

Pamoja na hayo, mtuhumiwa huyo amekamatwa na lita tano za gongo ambayo aliificha katika buti la gari yake ndogo, pia askari huyo amekamatwa na vyuma vinavyotumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali vikiwa vimehifadhiwa katika banda la bata kiasi cha ndoo mbili pamoja na madumu ya mafuta ya dizeli yaliyojaa mafuta na aliyaficha katika sebule yake.

 

Kihongosi amemwagiza OCD wa Arusha kumkamata mtuhumiwa huyo na kumfikisha katika vyombo vya sheria ili iwe funzo kwa wengine.

 

Katika oparesheni hiyo, Kihongosi aliambatana na OCD wa Arusha, OCCID pamoja na Meneja wa Tanesco Mkoa wa Arusha ambaye alifika na wahandisi wa Tanesco na kukata umeme uliokuwa umeunganishwa darini na swichi kuwekwa chooni kinyume na utaratibu ambapo vielelezo vyote vilichukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi.

 

 

Leave A Reply