Polisi Arusha waua wanafunzi
Abas Ally enzi za uhai wake
Na Joseph Ngilisho, Arusha
UTATA! Sintofahamu imegubika vifo vya wanafunzi wawili, Abas Ally (21) na Happines Ibrahim ‘Happy’ (19), wakazi wa jijini Arusha waliouawa kwa kupigwa risasi na askari polisi wakidhaniwa ni majambazi.
Happines Ibrahim ‘Happy’ enzi za uhai wake.
Tukio hilo lililoacha maswali mengi, lilijiri saa mbili usiku wa Oktoba 27, mwaka huu katika kizuizi cha mpakani mwa Mkoa wa Manyara eneo la Kibaoni, wilayani Karatu na Arusha ambapo wanafunzi hao walikuwa kwenye gari dogo aina ya Toyota Alteza.
Kwa mujibu wa shuhuda mmoja wa tukio hilo (jina linahifadhiwa kwa sasa), Abas na Happy walikuwa wanafunzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha City Media ngazi ya diploma mwaka wa kwanza na kwenye tukio hilo walikuwa na watu wengine wawili ambao majina yao hayakufahamika mara moja.
Chanzo kilisema kuwa, wakati wa tukio hilo, marehemu Abas ndiye aliyekuwa dereva wa gari hilo lenye rangi ya silva na mpenzi wake Happy alikaa siti ya mbele upande wa abiria.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, polisi katika kizuizi hicho walipata taarifa kwamba, gari hilo lilipakia majambazi, ndipo polisi walipoamua kupanga magogo na mawe katika kizuizi ili kuwanasa watu hao.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa, wanafunzi hao walipofika katika kizuizi hicho walikuta magari yamesimama barabarani sanjari na magogo, hivyo wakapata hofu kwamba ni majambazi waliokuwa na lengo la kuwateka.
“Ndipo walipogeuza gari lao kwa kasi na kuelekea barabara ya vumbi. Askari wawili waliokuwa eneo hilo waliwamiminia risasi na kusababisha kupoteza maisha ya wawili hao,” kilisema chanzo.
Taarifa zaidi zinadai kuwa, marehemu Abas alipigwa risasi kadhaa, moja ilifumua kichwa, mbili zilimfikia kwenye mguu wa kulia, nyingine kwenye bega la kulia huku Happy akipigwa risasi mbili kifuani.
Hata hivyo, vijana wawili waliokuwa wamekaa siti ya nyuma ya gari hilo ambao ni mvulana na msichana ambapo pia inadaiwa ni mtu na mpenzi wake, waliponea chupuchupu na kutoka salama katika gari hilo.
Manusura hao walichukuliwa na polisi hadi Kituo cha Polisi Manyara Kibaoni na kufanyiwa upekuzi ambapo hawakukutwa na chochote kinachoashiria ujambazi isipokuwa chupa ya pombe kali na bangi.
Baba mzazi wa marehemu Abas, Ally Ibrahim (Bob Ally) alisema marehemu mtoto wake hakuwahi kujihushisha na matukio yoyote ya uhalifu ila siku ya tukio alimwomba gari kwa ajili ya matembezi ya kawaida wilayani Karatu na alishangaa kupata taarifa kwamba mwanawe ameuawa akihushishwa na ujambazi.
“Naomba jeshi la polisi lifanye uchunguzi wa kina juu ya vifo hivi. Naamini haki itatendeka na ukweli utajulikana ili iwe fundisho kwa askari polisi wasiozingatia maadili ya kazi zao,” alisema mzee huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Liberatus Sabasi alikiri kupokea taarifa hizo na kueleza kuwa, tayari polisi imeanza uchunguzi wa tukio hilo.
“Tupo katika mazungumzo na familia za marehemu juu ya tukio hilo,” alisema Kamanda Sabasi huku kukiwa na taarifa kuwa, jeshi hilo linawashikilia askari wake watatu kuhusiana na tukio hilo.