Polisi wa Kituo cha Buguruni jijini Dar wako hatarini baada ya kufungiwa huduna za kijamii kituoni hapo na aliyekuwa kigogo mmoja wa ngazi ya juu wa kanda maalum bila kufuata utaratibu.
Wakizungumza na mwandishi wetu wiki iliyopita baadhi ya polisi ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini kwa sababu za kiusalama walisema kwamba maisha yao yako hatari kutokana na kufungiwa huduma za kijamii kama kantini na duka kwani sasa wamekuwa wakipata vyakula na vinywaji uraiani na siyo kituoni hapo kama zamani.
“Hapa kituoni ni kama kambini kwa sababu kuna nyumba na tunaishi na familia zetu, kulikuwa na duka la bidhaa, kantini kwa ajili ya vinywaji na steshenari kwa ajili ya kutoa kopi ambayo imekuwa ikiwasaidia ofisini lakini kwa sasa huduma zote zimefungwa bila sababu na inasemekana kwamba kigogo huyo anataka aendeshe yeye.
“Kwa nini maduka na kantini za polisi vituo vyote vya polisi katika jiji la Dar yanafanyakazi isipokuwa hapa Buguruni? Kwa sasa tunakula uraiani na hata tukihitaji maji ama soda tunakwenda kununua mitaani, hii ni hatari kwa maisha yetu,”alisema askari polisi mmoja.
Polisi hao wanamuomba Mkuu wa Polisi Tanzania IGP, Ernest Mangu (pichani) awasaidie kurejeshwa kwa huduma hizo kwani zilikuwa zikiwasaidia.
Kamanda wa Polisi Ilala, SACP ACP Lukas Mkondya alipoulizwa ofisini kwake wiki iliyopita alikiri kupokea taarifa hiyo na kuahidi kushughulikia.