The House of Favourite Newspapers

Polisi Handeni Wahitaji Kuendelea Kuwapa Mafunzo Madereva wa Bodaboda Kuepusha Ajali

0

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, limesema ipo haja kwa waendesha bodaboda wilayani humo kuendelea kupatiwa mafunzo ya usalama barabarani kupunguza ajali.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda zaidi ya 160, Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Handeni Inspekta Gwantwa Mwakisole amesema kuna changamoto ya uelewa wa sheria kwa vijana wengi wanaondesha pikipiki.

“Mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki ni muhimu sana hasa kwa vijana wanaondesha pikipiki katika barabara kubwa (kuu) za kuunganisha mikoa kwani magari ni mengi na yanapita kwa kasi kubwa,” amesema.

Amefafanua kuwa vijana wengi wanaopita katika barabara kuu wanagongwa na magari hivyo njia pekee ya kuwapusha na ajali hizo ni kuwapatia mafunzo ya elimu ya usalama barabarani na kuwaomba Amend kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswis nchini kuendelea kutoa mafunzo hayo.

“Kampeni hii ya elimu ya usalama barabarani inayoratibiwa na Shirika la Amend kwa ufadhili wa ubalozi wa Uswiss nchini imefika katika Wilaya yetu ya Handeni na tunaona haja ya elimu hii kuendelea kutolewa kwa vijana wengi zaidi.

“Tuko tayari kupokea mafunzo haya na tunaomba Amend waje kuweka kambi hapa Handeni na sisi Jeshi la Polisi tutawapa ushirikiano mzuri kwani mafunzo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali za waendesha pikipiki,” amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa Amend Tanzania, Ramadhan Nyanza amesema jumla vijana 160 wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani sambamba na mafunzo ya utoaji huduma ya kwanza inapotokea ajali.

Ameongeza mafunzo hayo ni mwendelezo wa kampeni ya kuhakikisha vijana hasa waendesha bodaboda wanakuwa salama wawapo barabarani huku akisisitiza changamoto kubwa ni waendesha bodaboda wengi kutofuata sheria za usalama barabarani, hivyo kusababisha ajali zinazokatisha maisha au kusababisha ulemavu wa kudumu.

Leave A Reply