Polisi Kata Nchi Nzima Kupewa Pikipiki Ili Kuimarisha Usalama
Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Serikali inaendelea kuboresha utendaji kazi wa Polisi Kata na Shehia kwa kuwajengea vituo vya Polisi na kuwapatia vitendea kazi kama pikipiki Nchi nzima katika kutekeleza majukumu yao.
Waziri Masauni ameyasema hayo leo Oktoba 22, 2024, Mkoani Geita Katika hafla ya kukabidhi pikipiki 50 zenye thamani ya Tsh Milioni 175 zilizotolewa na mgodi wa Geita Gold Mine (GGML) ambapo amesema Serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na Polisi Kata / Shehia kwani wamesaidia sana kuimarisha usalama katika jamii.
Aidha Waziri Masauni amesema “Serikali ya awamu ya Sita kupitia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya mwaka 2024/2025 imepanga na kutenga bajeti ya Bilioni 224 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili kukamilisha, kuendeleza na kuanza ujenzi wa ofisi, vituo na makazi ya askari na kuongeza vitendea kazi vya kisasa katika kutoa huduma ikiwemo magari, pikipiki, boti na helkopta”.
Vilevile “Hadi sasa, Serikali imenunua Magari 384 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za Polisi kuanzia Makao Makuu ya Polisi hadi Wilaya na pikipiki 107 kwa ajili ya Polisi Kata na Shehia nchi nzima ikiwa ni lengo la Serikali kuhakikisha Jeshi la Polisi linapata vitendea kazi vya kutosha katika ngazi zote”. Aliongeza Waziri Masauni
Katika hatua nyingine Waziri Masauni amewapongeza mgodi wa Geita Gold Mine (GGML), na wadau wote ambao wamekuwa wakishirikiana na Wizara kupitia Jeshi la Polisi kwa kutoa michango mbalimbali ya kulizesha Jeshi hilo kutimiza majukumu yake ya kusimamia usalama wa raia na mali zao.
Naye Makamu wa Rais wa Geita Gold Mine, Terry Strong amesema anatarajia pikikipi hizo zitumike katika utoaji huduma za Polisi kwa wananchi kwa maeneo ambayo yamekuwa hayafikiki kwa urahisi.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela ameshukuru mgodi huo kwa namna ambavyo wamekuwa wakitumia sehemu ya faida yao kuboresha taasisi za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi ambapo leo Kukabidhiwa pikipiki 50.
Pia Mkuu wa Sera Mipango na Bajeti wa Jeshi la Polisi, SACP Justus Kamugisha ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, amesema pikipiki hizo zinakwenda kusaidia Polisi Kata 50 huku akibainisha kuwa Mkoa huo unaidadi ya Kata 123.