The House of Favourite Newspapers

Polisi kuuana Mwanza, mapya yaibuka

0

Kuaga (1)
Na Mwandishi Wetu, UWAZI
MWANZA: Bado Jiji la Mwanza limegubikwa na sintofahamu ya Polisi PC Daudi Elisha mwenye namba H 852 kumuua kwa kumpiga risasi askari mwenzake, PC Petro Matiko mwenye namba H 5990 kisha naye kujiua, mapya yameibuka.

Tukio hilo lililoitingisha Mwanza lilijiri saa 8 mchana wa Desemba 23, mwaka huu nje ya Benki ya Posta Tawi la Pamba.

Akizungumza na gazeti hili, kijana mmoja ambaye anadai alikuwa na ukaribu na PC Elisha, huku akiomba hifadhi ya jina lake, alisema anachokijua yeye kuhusu kisa cha mauaji hayo ni zaidi ya mchezo wa upatu.

Kuaga (4)“Watu wanasema walikuwa wakicheza upatu, Matiko akakosa kufuata makubaliano, ndiyo Elisha akakasirika na kumuua, lakini wiki moja kabla ya mauaji, Elisha aliniambia ana kitu kikubwa anataka kukifanya kwa Matiko.

“Nilimuuliza ni kitu gani, akasema ni sapraizi. Hakuniambia ataua. Kwa vile nilikuwa najua wanacheza upatu, sikupeleka mawazo kwamba sapraizi hiyo ni kumuua mwenzake.

“Kuhusu sababu ya upatu, inaweza kuwa kweli lakini nijuavyo mimi, Elisha alikuwa na ukaribu na dada mmoja anaitwa Jema lakini huyo dada pia alikuwa na mazoea na Matiko. Elisha amekuwa akimtaka Matiko kuacha mazoea na dada huyo lakini bila kuweka wazi kama yeye ni mpenzi wake au la!

Kuaga (5)“Siku moja kabla ya tukio mchana, Matiko na Elisha walikutana mjini, wakapishana Kiswahili tena. Elisha aliniambia amepishana Kiswahili na Matiko kuhusu huyo dada. Lakini Matiko amekuwa akimuuliza mwenzake kama yeye ni mpenzi wa huyo dada ila jamaa akawa hatoi jibu la wazi.

“Siku hiyohiyo, jioni yake, Elisha alimtuma mtu kwenda kwa Matiko akimtaka amlipe pesa zake alizomkopesha kiasi cha shilingi laki mbili (200,000) na alimpa masaa matatu tu. Lakini inaonekana Matiko aliamini pesa hizo siyo sababu ya Elisha kumpa masaa matatu, bali kisa kinatokana na ukaribu na huyo dada.

“Na yeye alimrudishia ujumbe kwa mtu huyohuyo akimwambia Elisha kwamba, kama anadai kwa masharti hatamlipa lakini kama anadai kistaarabu, atazipata na si kwa masaa matatu, bali kesho yake akienda benki,” alisema kijana huyo.

Akaendelea: “Sasa nilipokuja kusikia kwamba, Elisha amempiga risasi Matiko mpaka amefariki dunia naye kajiua, nilishtuka sana. Nikakumbuka ile sapraizi aliyoniambia Elisha. Kwa hiyo naamini kama ni kumuua Matiko, Elisha alishapanga muda, halikuwa wazo la ghafla.

Kuaga taaluma (1)“Wakati wa msiba, kuna afande mmoja aliniambia siku ya tukio, Matiko alipokuwa anakwenda benki, yeye alikuwa akimsubiri mahali lakini Matiko alimwambia anahisi mwili hautaki kutembea. Akamwambia asiende benki, anaweza kupata ajali. Wao waliwaza ajali ya kugongwa na gari lakini Matiko alimwambia binadamu amepangiwa kila kitu katika maisha yake yote.

“Matiko alisema hata asipokwenda benki, kama siku hiyo ni ya kupata ajali, ataipata popote, hata akiwa amelala chumbani,” alisema kijana huyo.

TUJIKUMBUSHE
Siku ya tukio, afande Matiko alifika kwenye benki hiyo akiwa kavaa kiraia kwa lengo la kuchukua fedha. Lakini baada ya muda alitoka na kuwaambia maafande waliokuwepo kwenye lindo ambao ni Elisha na PC Remigius Alphonce (H 4291) kwamba, ameshindwa kutoa fedha kutokana na mtandao kuwa chini.

Kuaga taaluma (2)Lakini kabla hajaondoka, PC Elisha alikoki bunduki na kuweka risasi chemba. Afande Alphonce alimuuliza kisa cha kuweka risasi chemba wakati hakuna hali ya hatari, akamjibu asifuatilie mambo yake.

Ilikuwa kufumba na kufumbua, Elisha alimfyatulia risasi Matiko. Iliingia begani na kutokea mgongoni. Na yeye alijifyatulia chini ya kidevu na kutokea kisogoni. Alifariki dunia palepale huku Matiko akifia Hospitali ya Bugando.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema chanzo hakijajulikana huku jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi.

Mwili wa PC Matiko ulisafirishwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenda kwao mkoani Mara kwa mazishi na mwili wa Elisha ulisafirishwa kwenda Bariadi, Simiyu kwa mazishi.

Leave A Reply