Polisi Moro Yamsaka Dereva wa Gari la Taka iliyosababisha Watu Wawili Kufariki
Watu wawili wamepoteza maisha na wawili kujeruhiwa vibaya baada ya gari la kubeba taka aina ya Isuzu Tiper lenye namba za usajili T 882 DQJ kuacha njia na kuwagonga wafanyabiashara waliokuwa wamepanga bidhaa zao pembeni mwa barabara kuu ya Morogoro – Dodoma eneo la Kihonda Maghorofani, Manispaa ya Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, dereva wa gari hilo alishindwa kulimudu baada ya mfumo wa breki za gari kuharibika, hali iliyosababisha kugonga pia bajaji yenye namba za usajili MC 445 DRG. Aidha, dereva huyo ametoweka na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka.
Waliofariki katika ajali hiyo wametambuliwa kuwa ni Lisa Zakaria Josia (20) na Habibu Shabani Nassoro (63). Wakati huo huo, majeruhi ni Paul Vitalis Temba (71) na Josephiner Francis Mbago (48) ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.
Kamanda Mkama ametoa wito kwa wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo, kuacha kupanga bidhaa zao kando ya barabara ili kuepuka matukio ya ajali kama hili. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa uharibifu wa mfumo wa breki wa gari ya taka ndiyo chanzo cha ajali hiyo mbaya.
Ajali hiyo imetokea Septemba 28, 2024, jioni, kwenye makutano ya barabara ya Morogoro-Dodoma, ambapo gari hilo lilienda kugonga wafanyabiashara hao wakiwa kwenye biashara zao kando ya barabara. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi huku likitoa wito wa tahadhari kwa wananchi na kuhakikisha usalama wao wakiwa katika maeneo ya biashara.