Polisi mwanamke alivyoteketea moto na mchepuko wake

Stori: Mwandishi Wetu, UWAZI
RUKWA: Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani wa kike, Atuganile Mwakibete (37) na mpenzi wake (mchepuko), Sunday Mhagama (36) wameteketea kwa moto baada ya nyumba waliyokuwa wamelala kuungua.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, SACP Jacob Mwaruanda aliliambia gazeti hili kuwa tukio hilo lilitokea Februari 2, mwaka huu saa saba na robo mchana katika Mtaa wa Maporomoko, Kata ya Laela, Wilaya ya Kipolisi ya Laela mkoani hapa.

Alisema nyumba iliyoteketea kwa moto ambayo askari huyo wa kike alikuwa amepanga ilikuwa ni mali ya Yaiyela Mwamahonje, hata hivyo, watoto wa wawili wa polisi huyo walinusurika kifo licha ya kuwemo ndani ya nyumba hiyo wakati ajali inatokea.
Alifafanua kuwa, Mhagama aliyekuwa rafiki wa askari huyo ni mkazi wa Mbeya ambako mkewe anaishi na alikuwa na mazoea ya kumtembelea mpenzi wake huyo aliyekuwa ameachana na mumewe wa ndoa.

“Vyumba viwili, yaani sebule na chumba walichokuwa wamelala marehemu viliwaka moto baada ya jenereta lililokuwa likifanya kazi likiwa sebuleni kulipuka na kuwajeruhi vibaya,” alisema Kamanda Mwaruanda.

Kamanda huyo aliongeza kuwa, Atuganile alifariki dunia Februari 8, mwaka huu saa 2.30 asubuhi alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga ambapo Mhagama alikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya mjini ambako alifariki dunia Februari 9, mwaka huu na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Loading...

Toa comment