Polisi waivamia Benki ya Baclays

 

KIKOSI cha polisi wa dharura nchini Kenya wamevamia benki ya Barclays iliyopo katikati mwa mji huo kwa msako wa watu wanaowalaghai watu kwa pesa bandia.

 

Kikosi hicho maarufu kinachojulikana kama Flying Squad kimekuwa kikilisaka kikundi cha watu wanaoaminiwa kuwalaghai watu na kuwapatia watu pesa bandia.

Wakiongozana na wapelelezi kutoka Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), maofisa hao wanaripotiwa kuwepo kwenye benki hiyo huku ripoti zikisema kuwa wateja wa benki hiyo walikuwa wamewasilisha kiwango kikubwa cha pesa bandia.

 

Dola hizo bandia zinakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi za Kenya bilioni 17. Mkuu wa kikosi cha polisi cha dharura, Musa Yego, amethibitisha kufanyika kwa uvamizi huo.

 

Taarifa ya benki hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari imethibitisha tukio hilo. Wakenya watatu na raia mmoja wa kigeni wamekamatwa, zimesema taarifa za vyombo vya habari nchini Kenya.

 

Jumanne polisi walikita kambi katika Benki ya Barclays tawi la Queensway mjini Nairobi kufanya uchunguzi wao dhidi ya kikundi hicho kilichovamia jiji.

 

Inasemekana kulikuwa na mteja ambaye hajatambuliwa ambaye amekuwa akiweka dola bandia kwenye hifadhi ya dola ya benki.

 

Inasemekana mtu huyo amekuwa akiwaleta watu wanaoweza kuwekeza  kwenye benki kushuhudia ‘ukarimu’ wake wa pesa na polisi wakashuku kuwa alikuwa katika njama za kuwaibia wafanyabiashara.

 

Alizingirwa na maofisa Jumanne asubuhi baada ya kuja kuangalia ‘utajiri wake’ wa thamani ya mabilioni ya shilingi za Kenya.

 

Shughuli katika benki zilivurugika kwa muda wakati wa tukio hilo, kutokana na msongamano wa watu waliokuwa wakishuhudia kilichotokea, kuwasili kwa magari kadhaa ya polisi, kuvamia kwenye ukumbi wa benki na kuanza msako wa malipo bandia.

 

Taarifa za tukio hilo zimetolewa na vyombo mbalimbali vya habari nchini Kenya. Benki huwapatia wateja wao vijisanduku salama kutunza nyaraka zao muhimu kama vile, vibali vya ardhi, vibali vya magari yao, vyeti, pesa za kigeni na vyeti vya elimu miongoni mwa nyaraka nyingine.

Uchunguzi huu unafanyika yapata mwezi mmoja baada ya maofisa kutoka kitengo maalam cha udhibiti wa uhalifu kukamata kiwango kikubwa cha pesa bandia za kigeni na za Kenya, zilizokuwa zimefichwa kwenye makazi ya mtu binafsi katika eneo la Ruiru viungani mwa mji wa Nairobi.

 

Polisi waliuambia mkutano wa waandishi wa habari kuwa pesa hizo feki zilikuwa sawa na shilingi bilioni 32 za Kenya. Baadhi ya pesa hizo zilikuwa ni Euro, Pauni, dola  na shilingi za Kenya.

 

Washukiwa hao ambao walikuwa ni mume na mke pamoja na mshirika wao katika biashara (mwanamke) walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Loading...

Toa comment