The House of Favourite Newspapers

Polisi Wanavyobebeshwa Mzigo Wa Lawama Za Wanasiasa

b78c82722al

 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu (kulia) akiongea jambo.

Na Walusanga Ndaki

KunA baadhi ya watu wanasema hakukuwa na haja ya kulipongeza au kulifurahia  tamko la majuzi la polisi la kuruhusu mikutano ya ndani ya vyama vya siasa ambayo lilikuwa limeifungia kwa karibu mwaka.
 
Ni kwa nini?  Ni kwa sababu upigaji marufuku wa mikutano hiyo – uliovibana wa vyama vya upinzani tu – ni jambo ambalo halikuzingatia haki na katiba ya nchi, mbali na kwamba lilifanywa kwa upendeleo na kwa sababu ambazo hazikukubalika kwa pande zote husika.  

Kwa kifupi na kwa mujibu wa maadili na weledi wa kikazi (professionalism),  jeshi la polisi katika kuzuia mikutano hiyo,  lilikuwa linafanya kazi ambayo si yake, mbali na kutoa sababu ambazo ziliwashangaza watu wengi wenye kufuatilia siasa za nchi hii.  

Machoni na katika akili za Watanzania, jeshi la polisi ambalo msingi wake ni kulinda furaha na amani ya Watanzania wote, limejikuta likilalamikiwa na wananchi wote wenye nia njema na nchi hii kwa kufanya kazi kufuatana na matakwa na maelekezo ya wanasiasa! Matokeo yake, jeshi hilo limejikuta likibeba mzigo wa lawama ambao ulikuwa ubebwe na wanasiasa!

Yote kwa yote, matokeo ya mkanganyiko unaojenga taratibu hisia za chuki baina ya jeshi la polisi na wananchi ni mipangilio yetu ya kisiasa ndani ya nchi hii ambapo katiba imewapa wanasiasa nguvu kubwa kuliko wataalam wetu, wakiwemo polisi.  Kwa uwazi zaidi ni kwamba wanasiasa ambao wana mamlaka ya kuwaajiri (kwa kuwateua) na kuwafukuza wataalam nchini, ndiyo wenye nguvu ya mwisho katika maamuzi.

Katika mazingira kama haya, si rahisi wataalam au wasomi wa nchi hii kufanya kazi kwa uhuru na kwa weledi unaotakiwa, bila ya kutia maanani matakwa ya wanasiasa.  

Kinachotokea ni kwamba, wakati wanasiasa wakiwa ‘wametulia’ mahali fulani, wataalam wa nchi hii ndiyo hubeba mzigo wa chuki za wananchi kwa kulazimika kupindisha maadili ya kazi zao.

Jeshi la polisi chini ya mkuu wake, IGP Ernest Mangu (pichani) ni kimbilio la mwanzo kabisa kwa mwananchi yeyote katika kutafuta haki – kabla hata ya kupitia kwa mjumbe wa nyumba kumi au hata serikali za mitaa – ni lazima lizingatie ‘professionalism’ yake ili liendelee kuheshimiwa na mamilioni ya wananchi na wanasiasa wa nchi hii ambayo siku zote tumekuwa tukisema imejaa amani na utulivu.

Ili tuheshimiane na kuishi kwa upendo, lazima wataalam na wasomi wetu wasisahau kwamba tunaamka kila siku asubuhi kwenda kazini kuijenga nchi yetu ili iwe urithi wa furaha kwa vizazi vijavyo, si kwa kuwajengea chuki na matabaka ambayo baadaye yatasababisha kuibomoa na kuirudisha nyuma kwa miaka 50!

Tunaamka kila siku asubuhi kwenda kazini kujenga furaha kwa wote si kwa kuwafurahisha watu wachache na kuwaacha mamilioni wamenuna na wakisononeka au wakiwa rumande au gerezani bila sababu za msingi. Huo ni uonevu wa wazi. Ni dhambi kwa Mungu!
Jeshi la polisi ambalo lina wataalam na wasomi wengi, ambalo ni kizazi cha Watanzania wengi maskini walioko vijijini, lisiache kuendeleza kazi yake nzuri kwa wananchi,  likifanya hivyo bila upendeleo na likikwepa kupakwa matope kutokana na utashi au matakwa ya watu wachache.

Kinachotakiwa kufanyika leo ni kujenga mazingira ambayo yatamwezesha kila Mtanzania – wakiwemo polisi na wataalam wote – kuishi kwa furaha leo, kesho na keshokutwa bila hofu, bila kutembea tukishituka na kugeuka nyuma kila mara.
Kwa kufanya hivyo jeshi la polisi litaendelea kuombewa baraka na wananchi wote!

Comments are closed.