Polisi Watoa Taarifa Mgombea Wa Chadema Aliyefariki Baada Ya Kupiga Kura – Video
Jeshi la Polisi Tanzania limetoa ufafanuzi kuhusu taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Ndg Modestus G Timbisimilwa ambaye alikuwa Mgombea Ujumbe Mchanganyiko wa Mtaa na Wakala wa Nje wa CHADEMA kuwa ameuawa na kutelekezwa na Polisi.
Taarifa ya leo Novemba 27, 2024 iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Dodoma, DCP, David A. Misime imebainisha kuwa leo Novemba 27,2024 majira ya saa 2:10 Modestus G Timbisimilwa alifika katika Kituo cha Kupigia kura cha Ulongoni A. Gongolamboto Jimbo la Ukonga na kuelekea kituo namba 5 akiwa anafuatilia masuala ya uchaguzi.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza mwamba Timbisimilwa alianza kujisikia vibaya na kusema anahisi “presha”. Antony John Mjelwa wa Chadema alimpa msaada na kumpeleka Kituo cha Afya cha Mongolandege na wakati anapatiwa huduma za kitabibu akapoteza maisha. Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali kusubiri taratibu zingine kukamilishwa.