Polisi Watumia Mabomu ya Machozi Kutawanya Maandamano ya Kupinga Kodi na tozo Kenya
Polisi nchini Kenya wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika mji mkuu wa Nairobi wanaopinga baadhi ya hatua zinazopendekezwa na serikali za kutoza ushuru mpya au wa juu zaidi kwa bidhaa zikiwemo mafuta.
Mojawapo ya hatua kuu zinazopingwa katika muswada wa fedha ambao unapingwa na wengi ni tozo mpya ya 3% ya nyumba kwa wafanyakazi wote wanaolipwa mishahara na kuongeza ushuru wa ongezeko la thamani kwenye mafuta hadi 16%.
Muswada huo pia unataka kodi kwa bidhaa za urembo, sarafu za mtandani na mapato yatokanao na mitandao ya kijamii. Ni miongoni mwa hatua ambazo zimepingwa na Wakenya wengi.
Makumi ya waandamanaji walikuwa wakijaribu kukusanyika katika bustani moja katikati mwa jiji la Nairobi kabla ya kuandamana hadi bungeni kuwataka wabunge kukataa mapendekezo hayo.
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa baadhi ya waandamanaji walikamatwa. Wabunge wanatazamiwa kujadili mswada huo siku ya Alhamisi, huku kukiwa na onyo lililotolewa na Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua dhidi ya wanaopinga mapendekezo hayo.