The House of Favourite Newspapers

POLISI WAUA MTUHUMIWA WA UJAMBAZI DAR – VIDEO

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemuua kwa risasi mtu mmoja anayedaiwa kuwa jambazi maeneo ya Buza jijini humo wakati akijaribu kuwatoroka askari alipokuwa akienda kuwaonyesha sehemu walipoficha silaha na wenzake.

 

Akizungumza na wanahabari jijini Dar, RPC Lazaro Mambosasa amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na bastola na alipohojiwa alikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya ujambazi katika maeneo ya Mbagala na Kibiti.

 

“Machi 2018, tulipata taarifa kuwa maeneo ya Mbagala Kibonde-Maji kuna mtu anafanya matukio ya uhalifu kwa kutumia silaha, tulifanikiwa kumkamata na baada ya kumpekua alikutwa na bastola ndogo aina ya revolver  ikiwa na risasi sita.

“Tulipomhoji alikiri kuhusika na matukio ya ujambazi na kuwataja wenzake, aliahidi kutupeleka wanapoficha silaha maeneo ya Buza. Baada ya kukaribia eneo wanapoficha silaha hizo alianza kupiga makelele na kukimbia akijaribu kuwatoroka askari, walipomwamuru asimame  alikaidi.

 

“Polisi walifyatua risasi moja iliyompata na kumjeruhi, baadaye alipoteza maisha na mwili wake kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi na kuhifadhiwa. Lakini wenzake tunawasaka kwa sababu aliwataja kwa majina na mahali wanapoishi.”

 

Pia jeshi hilo linamshikilia Majid Abdallah (31) aliyekamatwa na bastola akiwa ameificha uvunguni mwa kitanda. Mambosasa amesema uchunguzi wa kesi hiyo unaendelea na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara moja.

 

Comments are closed.