Polisi Yapiga marufu matumizi ya silaha aina ya gobore kwenye shuguli za ulinzi
Jeshi la Polisi Nchini limepiga marufu matumizi ya silaha aina ya gobore kwenye shuguli za ulinzi huku Jeshi hilo likisema kuwa kutokana na suala la umiliki wa Silaha za Moto limeona ni vyema kuwafahamisha watanzania masuala matano yanayohusiana na umiliki wa silaha hizo hapa Nchini.
Akitoa taarifa hiyo leo Juni 28 Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema kuwa Kampuni binafsi za ulinzi kutumia silaha zilizotengenezwa kienyeji (Gobore) kinyume cha Sheria.
DCP Misime ameongeza kuwa Mtakumbuka kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria Namba 2 ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015 sambamba na kufuta Sheria ya Silaha na Risasi ya Mwaka 1991 kwa lengo la kukidhi mahitaji ya sasa ya kukabiliana na changamoto za kumiliki na kusambaa kwa silaha haramu.
Aidha amebainisha kuwa Kutungwa kwa Sheria hii kulikwenda sambamba na marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa sura ya 290 kwa kuondoa kifungu 7(1) (L) kilichokuwa kinazipa Halmashauri na Manispaa Mamlaka ya kukusanya mapato yatokanayo na leseni za silaha aina ya Gobore ambapo kufuatia kutungwa kwa Sheria mpya, jukumu hili lilipewa Jeshi la Polisi.
Sambamba na hilo amesema katika siku za karibuni, Jeshi la Polisi Nchini limebaini kuwepo kwa baadhi ya kampuni binafsi ya ulinzi ambayo yanamiliki silaha aina ya Gobore bila kuwa na vibali kinyume na utaratibu wa sheria unaozitaka kampuni za ulinzi kumiliki shotgun kwa ajili ya shughuli za ulinzi.
Msemaji wa hilo aliendelea kusema kuwa wananchi waliokuwa wakimiliki silaha aina ya Gobore kwa kutumia leseni zilizotolewa na Halmashauri za Miji na Manispaa, walielekezwa kuendelea kulipia silaha zao katika Ofisi za Wakuu wa Polisi Wilaya (OCD) mpaka watakapoamua kutoendelea kumiliki au kutokana na sababu nyingine ikiwemo kufariki na kwamba silaha hizo hazitamilikishwa kwa watu wengine tena bali Jeshi la Polisi litaziondosha kwa kuziteketeza.