Potter Kuongea na Wamiliki wa Klabu ya Chelsea Wakati wa Kombe la Dunia
KOCHA mkuu wa klabu ya Chelsea Graham Potter amesema atayatumia mapumziko ya kupisha mashindano ya Kombe la Dunia nchini Qatar 2022 kuongea na wamiliki wa klabu yake ili kuona namna ya kufanya maboresho kwenye kikosi chake kuelekea dirisha dogo la usajili la mwezi Januari.
Potter alihamia katika klabu hiyo akitokea katika klabu ya Brighton ikiwa ni baada ya Chelsea kumtimua kazi Kocha raia wa Ujerumani Thomas Tuchel baada ya klabu hiyo kufanya vibaya katika mchezo wa kwanza wa Klabu Bingwa Barani Ulaya na pia kuwa na mwenendo mbaya kwenye Ligi Kuu ya EPL.
Licha ya kufanikiwa kuipeleka klabu hiyo katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa lakini Potter na Chelsea kwa ujumla wamekuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa siku za hivi karibuni katika michezo ya Ligi Kuu ya Epl huku leo ikiwa na kibarua Kizito cha kupambana na Newcastle United iliyopo kwenye kiwango cha hali ya juu huku ikiwa katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ya Epl hadi sasa.
“Hakika, tunatakiwa kufikiria nini kimetokea lakini pia tunatakiwa kufikiria nini tunatakiwa kufanya ili kuimarisha kikosi.” alinukuliwa Potter alipoulizwa endapo kipindi cha mapumziko kupisha Kombe la Dunia anaweza kukitumia kuongea na wamiliki wa klabu hiyo ili kuimarisha kikosi hicho katika majira ya usajili wa dirisha dogo mwezi Januari.