The House of Favourite Newspapers

Prof. Kabudi Akanusha Azory Gwanda Kufariki Dunia

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amekanusha kuwa amethibitisha ‘kifo’ cha mwanahabari Azory Gwanda.

Msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania, Dkt Hassan Abbas amemnukuu Profesa Kabudi kwa kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter akisema:

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa potofu zinazoendelea kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii ikinukuu kimakosa mahojiano yangu kwenye kipindi cha BBC FOCUS ON AFRICA zikidai kuwa nimethibitisha kwamba mwanahabari Azory Gwanda amefariki dunia.”

Lakini Prof Kabudi pia amesema bado haijulikani kama Bw Gwanda yungali hai: “Mpaka sasa hakuna uthibitisho kuwa Azory yuko hai au amefariki. Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuchunguza tukio hilo na matukio mengine yaliyotokea katika machafuko ya Kibiti, Pwani yaliyosababisha ama watu kadhaa kupoteza maisha au kupotea.”

Kabudi amesema kuwa, kilichotokea ni tafsiri potofu ya kile alishokisema: “Hii sio tafsiri sahihi kuhusu kile nilichokisema. Katika mahojiano hayo nilieleza kuwa tukio lililotokea Kibiti lilikuwa ni la kuhuzunisha na wapo watanzania waliouawa na wengine kupotea. SIKUTHIBITISHA kuwa Azory Gwanda amefariki.”

Comments are closed.