The House of Favourite Newspapers

Prof. Kabudi Asaini Mkataba Ujenzi Bomba la Mafuta Uganda Hadi Tanzania

0
Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Profesa Paramagamba Kabudi (kulia) na Waziri wa Nishati wa Uganda, Bi. Irene Muloni (kushoto) wakitia saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania, tukio lililofanyika leo katika Hoteli ya Serena, Kampala, Uganda.

Na Benny Mwaipaja, WFM.

Serikali za Tanzania na Uganda zimetiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania lenye urefu wa Kilometa 1,443, uliokadiriwa kugharimu zaidi ya Dola bilioni 3 nukta 55, mjini Kampala Uganda, leo.

Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Profesa Paramagamba Kabudi (kulia) na Waziri wa Nishati wa Uganda, Bi. Irene Muloni (kushoto) wakitia saini Mkataba huo.

Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Profesa Paramagamba Kabudi na Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhandisi Irene Muloni.

Ujumbe wa Tanzania na Uganda ukishuhudia tukio la utiwaji saini wa Mkataba huo.

Tukio hilo limekuja siku chache baada ya Marais wa Nchi hizo mbili, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni, kutia saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano ya vipengele vya mkataba, Ikulu Jijini Dar es salaam.

Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Profesa Paramagamba Kabudi, akihutubia baada ya kutia saini Mkataba huo.

Hafla ya kutia saini Mkataba huo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, Jijini Kampala, Uganda imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wanasheria Wakuu wa Serikali, Wakurugenzi na Viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusika katika mradi huo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Bw. George Masaju (kulia) na Mwanasheria wa Uganda Bw. Milliam Byaruhanga (kushoto), wakionesha nakala za Mkataba huo.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Tanga Tanzania, unatarajia kusisimua uchumi wa nchi hizo mbili na katika mchakato wa ujenzi wake zaidi ya watu 10,000 wanatarajiwa kunufaika na ajira.

Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Profesa Paramagamba Kabudi (kulia) na Waziri wa Nishati wa Uganda, Bi. Irene Muloni (kushoto) wakionesha Mkataba huo.

Hivi Karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliuelezea mradi huo kuwa ni mkubwa kwakuwa Uganda imegundua shehena kubwa ya mafuta katika eneo la Hoima kiasi cha mapipa bilioni 6 na laki 5 na kwamba Tanzania inatarajia pia kupata mafuta kule ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, ambayo yatapitishwa katika bomba  hilo hilo.

Leave A Reply