Prof Kitila: Kuna Haja ya Kutengeneza Sera za Uagizaji Magari Kulinda Viwanda vya Ndani

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof Kitila Mkumbo amesema kuna haja ya kurekebisha Sera katika sheria za uagizaji wa magari ili kulinda viwanda vya utengenezaji magari nchini.
Ameyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza magari nchini cha GF Vehicle Assemblers (GFA) kilichopo Kibaha mkoani Pwani.
Akiwa ameambatana na viongozi wa TCI, Waziri Mkumbo alitembelea kiwanda hicho na kujionea namna weanavyounganisha magari hayo kuanzia hatua ya mwazo mpaka linakamilika na alifanikiwa kushuhudia uzinduzi wa gari ya 3400 ikiwa ni tangu kuanzishwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Ezra Mereng aliwasilisha hoja ya maombi kwa serikali ya kubadilishwa kwa sera na sheria za uagizaji wa magari nchini ili kulinda viwanda vya ndani.
Alisema wao kama kampuni wanafanya upanuzi wa kuingia awamu ya 3 ambayo inategemewa kufanya uwekezaji wa mtaji wa zaidi ya bilioni 10 na mpaka sasa imeajiri zaidi ya vijana 200 na katika awamu ya 3 wanatarajia kuajiri zaidi ya vijana 300 wa ajira ya moja kwa moja.
Katika awamu hii tunahitaji vitu vingi vipatikane nchini kama vile chuma na vifaa vingine kwa mfano tumeshaanza kununua betri za magari kutoka katika kiwanda kimoja cha hapa nchini sasa bila kufanyika kwa mabadiliko ya sheria za kulinda viwanda vya ndani ni kazi bure.
Kwa sasa kumekuwa na uagizaji holela wa magari na katika hili, Tanzania tunakuwa walaji wa mwisho kwa kuwa magari mengi ni ya mtumba (used) Pia kukiwa na sheria ya manunuzi na usimamizi kwa miradi mikubwa ya nchi basi lazima magari au vifaa vitakavyotumika vinunuliwe nchini, hii itasaidia kuvilinda viwanda vyetu, alimaliza kusema Ezra.