Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ameipongeza taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa kuendeleza juhudi za kusaidia watoto wa familia zenye uhitaji kwa kugawa sare na vifaa vya shule, akisema hatua hiyo inaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha elimu jumuishi na bora kwa wote.
Mkenda ametoa pongezi hizo wakati wa hafla ya kugawa sare na vifaa vya shule kwa watoto 400 kutoka vituo saba vya makao ya watoto jijini Dar es Salaam vilivyotolewa na taasisi ya LALJI FOUNDATION ikiwa ni sehemu ya taasisi hiyo kuunga mkono juhudi za Serikali kuinua elimu kwa watoto kutoka familia zenye uhitaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mkenda amesema hatua hiyo ya kusaidia watoto walio katika mazingira magumu inaonyesha mshikamano wa taasisi binafsi na Serikali katika kuhakikisha elimu inapatikana kwa usawa na bila ubaguzi.
“Watoto hawa sasa watajiunga na wenzao mashuleni wakiwa na furaha na hali ya kujiamini Watakuwa na sare, mabegi, viatu na vifaa vya kujifunzia sawa na wenzao. Hii ni hatua muhimu katika kuondoa unyonge na kuleta matumaini mapya kwa watoto hawa,” alisema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake, Kamishna wa Elimu Tanzania Lyabwene Mutahabwa alisema msaada huo utapunguza changamoto zinazowakabili watoto katika kuanza mwaka wa masomo.
“Watoto hawa sasa watahudhuria shuleni kwa wakati, bila kubeba mzigo wa kutafuta sare au vifaa. Hii itaongeza mahudhurio na hatimaye kuongeza ufaulu,” alisema Mutahabwa.