PSG, Real Madrid na Chelsea Zapigana Vikumbo kwa Beki wa RB Leipzig
KLABU za Paris Saint Germain, Real Madrid na Chelsea zinatunishiana misuli ya fedha kwa kumuwania mlinzi wa kati wa klabu ya RB Leipzig na Timu ya Taifa ya Croatia Josko Gvardiol.
Gvardiol (20) amekuwa katika rada za Chelsea kwa muda mrefu, ambapo majira ya dirisha la usajili la kiangazi Chelsea ilituma ofay a zaidi ya paundi milioni 80 kutaka kumsainisha Gvardiol mkataba wa awali utakaomfanya ajiunge na klabu hiyo msimu wa 2023/2024 lakini RB Leipzig ilikataa dili hilo na kumuongeza Gvardiol mkataba mpya.
Kwa sasa beki huyo anayefanya vizuri akiwa na timu ya Taifa ya Croatia katika mashindano ya Fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar anaonekana kama mbadala wa Milan Skriniar kwa upande wa PSG ambapo Luis Campos tayari amenza jitihada za kuangalia uwezekano wa kuinasa Saini ya nyota huyo.
Katika mahojiano yake na Gazeti la The Telegraph la nchini Uingereza Gvardiol alibainisha kuvutiwa na uwezekano way eye kucheza ndani ya kikosi cha Graham Potter ingawa aliitaja Real Madrid kama moja ya klabu bora duniani na haitaji kuelezewa hilo na mtu mwingine yeyote yule.
Chelsea wanapewa nafasi kubwa ya kukamilisha uhamisho wa nyota huyo kutokana na kuwa na uhusiano mzuri na mabosi wa RB Leipzig hiyo ikiwa ni hivi karibuni kukubaliana katika dili la uhamisho wa nyota mwingine wa klabu hiyo raia wa Ufaransa Christopher Nkunku ambaye atajiunga na The Blues msimu ujao wa 2023/2024.