The House of Favourite Newspapers

PSG Yazima tambo za Man United

BAADA ya kutamba kwa muda mrefu hatimaye jana Manchester United walikutana na kisiki baada ya kuchapwa mabao 2-0 na PSG kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa.

 

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Dimba la Old Trafford, United waliingia uwanjani wakiwa na matumaini ya kuendeleza moto wa kocha wao Ole Gunnar Solskjaer wa kushinda mfululizo lakini mambo yakawa magumu.

 

 

Angel Di Maria ambaye mashabiki wa United walikuwa wakimzomea kuanzia mwanzoni mwa mchezo huo ndiye alikuwa mwiba kwao baada ya kutoa pasi zote mbili za mabao.

Bao la kwanza la PSG liliwekwa kimiani na Presnel Kimpembe ambaye alimalizia kona safi iliyopigwa na Muargentina huyo ambaye aliwahi kuwika akiwa na United katika dakika ya 53 ya mchezo.

 

Hata hivyo, United waliendelea kupambana wakiamiani kuwa wanaweza kurudisha bao hilo lakini walishangaa baada ya mshambuliaji hatari wa PSG ambaye anaaminika atakuwa Mchezaji Bora wa Dunia miaka michache ijayo, Kylian Mbappe kuifungia timu hiyo bao la pili.

 

Mbappe alifunga bao hilo katika dakika ya 60 ya mchezo baada ya PSG kupiga pasi mfululizo na mpira kumkuta Di Maria ambaye alimpasia Mfaransa huyo na kuuweka kimiani.

Hata hivyo, baada ya kuonywa mara nyingi, dakika ya 89 haikuwa nzuri kwa kiungo wa United, Paul Pogba baada ya kupewa kadi nyekundu ambayo itamfanya akose mchezo wa marudio wiki tatu zijazo.

 

Katika mchezo mwingine wa jana, Roma walifanikiwa kuichapa Porto mabao 2-1, leo Real Madrid watakipiga na Ajax huku Spurs wakivaana na Dortmund kwenye Dimba la Wembley.

Comments are closed.