PURA Yajivunia Mafanikio Kupitia Baraza La Wafanyakazi
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mh. Charles Sangweni amelipongeza baraza hilo kwa mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Mamlaka kutokana na utendaji wa baraza hilo.
Mh. Sangweni ameyasema hayo kabla ya kulivunja rasmi baraza hilo la kwanza katika kikao chake cha saba, kutokana na baraza hilo kufikia ukomo wake kwa mujibu wa mkataba ulioingiwa baina ya PURA na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE).
“Tunajivunia kazi kubwa iliyofanywa na baraza hilo katika kuchochea maendeleo ya taasisi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi na utekelezwaji wa majukumu mbalimbali ya PURA,” alieleza.
Aliongeza kuwa kutokana na ushirikishwaji huo, wafanyakazi wamepata motisha zaidi ya kufanya kazi kwa ari, ushirikiano na ubunifu na hivyo kuiwezesha taasisi kuendelea kutimiza majukumu yake katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli.
Mh. Sangweni alibainisha kuwa Baraza la Pili litaanza kazi rasmi Januari 2024 kwenye kikao chake cha kwanza ikiwa ni baada ya kufanyika uchaguzi wa wajumbe wapya kwa ngazi ya taasisi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania-TUCTA, Heri Mkunda amelipongeza baraza hilo kwa kazi waliyoifanya na kutoa pongezi mahususi kw menejimenti ya PURA kwa kuendelea kutengeneza mazingira bora ya kazi kwa wafanyakazi ili kuboresha utendaji wao.
Ametoa pia rai kwa wafanyakazi wa Mamlaka kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi mapana ya taifa kupitia sekta ndogo ya mafuta na gesi nchini.
“Mna wajibu mkubwa wa kufanya kazi kwa bidii, kwa kujituma na kushirikiana ili kutimiza malengo na majukumu yaliyokasimiwa kwa taasisi kwa mujibu wa sheria na miongozo ya nchi,” aliongeza.