The House of Favourite Newspapers

Pyramids Yabadili Beki Yanga SC

AKIWA na uhakika wa kucheza katika kikosi cha kwanza kitakachoivaa Pyramids FC ya nchini Misri, kocha msaidizi wa Yanga Mzambia, Noel Mwandila ameanza kumuandaa beki wa kati Mrundi, Moustafa Selemani.

 

Beki huyo pamoja na mshambuliaji Mkongomani, David Molinga waliikosa michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukosa leseni ya Caf kabla ya juzi kuhakikishiwa kucheza mechi na Pyramids baada ya kujibiwa barua yao.

 

Yanga inatarajiwa kucheza na Pyramids Oktoba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mkoani Mwanza kabla ya kurudiana kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano na kuthibitishwa na Mwandila ni kuwa amemuandaa beki huyo kwa ajili ya kuja kuziba nafasi ya beki wa kati au kulia ambayo yameonekana kuwa tatizo ndani ya kikosi hicho.

 

Yanga kwenye mechi yake ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Afrika walilazimika kumtumia beki Ally Ally ambaye anacheza beki wa kati kuitumikia nafasi hiyo kutokana na Paul Godfrey ‘Boxer’ lakini pia watamkosa beki Lamine Moro ambaye ana kadi nyekundu.

 

“Ni kweli kocha Mwandila amekuwa akimuandaa Mustapha kuja kucheza dhidi ya Pyramids kutokana na yeye kuwa na uwezo wa kucheza nafasi hizo vizuri.

 

“Tulimkosa kwenye mechi zile za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu alikosa leseni ya kucheza lakini sasa tuna uhakika wa kumuanzisha kwenye mechi hiyo na Waarabu na ndiyo maana kocha ameanza kumuandaa kucheza nafasi hizo kwa sababu ana uhakika wa kumtumia,” kilisema chanzo hicho.

 

Mustapha licha ya kusajiliwa kama beki wa kati akitokea Burundi lakini amekuwa akipangwa kama beki wa kulia ndani ya kikosi hicho na tayari ameshacheza kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting kufuatia kuumwa kwa Boxer.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.