The House of Favourite Newspapers

R.O.M.A, Darassa, Stamina Mwisho wa Ubishi Leo Dar Live

Roma Mkatoliki

MWISHO wa Ubishi! Unaweza kusema hivyo kwa maana nyingine katika siku hii ya Idd Mosi pale watakapovamia jukwaa moja la Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live wakali kibao wanaotikisa kwa michano Bongo wakiongozwa na R.O.M.A Mkatoliki, Darassa, Stamina na Mr Blue na kumaliza ubishi wa nani mkali wa michano.

Stamina

Akizungumzia shoo hiyo, Meneja na Mratibu wa Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar, Juma Mbizo alisema kuwa, shoo hiyo inatambulika kwa jina la Nishushe Dar Live ambapo wakali hao wataoneshana umwamba katika kutoa ‘freestyle’ na mashabiki ndiyo watakuwa majaji wa kuamua nani mshindi.

 

“Hii haijawahi kutokea Bongo na kwa mara ya kwanza sikukuu hii ya Idd Mosi mashabiki watashuhudia wakali kibao kama R.O.M.A, Stamina, Darassa na Mr Blue wakifanya ‘battle’ ya kihistoria tangu burudani izaliwe katika jiji hili la Dar,” alisema Mbizo na kuongeza:

 

“Wote tunajua kuwa R.O.M.A hapa kati alipata matatizo ya kutekwa na sasa yupo fiti kwa asilimia 200 hivyo mpambano utakuwa si wa kitoto ukichangia na Darassa naye ana ngoma mpya ya Hasara Roho na freestyle yupo vizuri, ukija kwa Blue na Stamina ni moto mwingine, yaani kifupi nikuachie wewe shabiki uje kuamua mshindi,” alisema Mbizo.

 

Burudani kwa watoto

Mbizo alisema kuwa, pazia la burudani kwa watoto litafunguliwa mapema kuanzia saa 2:00 za asubuhi ambapo kutakuwa na michezo mingi kama vile kubembea, kuteleza, kuogelea, michezo ya treni, ndege na mingine kibao.

“Watoto pia watapata burudani kutoka Kundi la Muziki wa Asili la Makhirikhiri kutoka Tanzania, Wakali wa Sarakasi, Wakali Dancers pamoja na mkali wa vichekesho, Bambo atakayehakikisha amevunja mbavu watoto wote,” alimaliza Mbizo.

 

Snura

Snura, Zanzibar Stars ndani

Ili kuweka mzani wa burudani sawa, Mbizo alisema kuwa, jukwaa litamalizwa na mkali wa Muziki wa Mduara anayebamba na ngoma kibao ikiwemo Ushaharibu, Chura, Najibadua, Shindu na nyingine kibao.

“Sikukuu hii, Snura atawaonesha live mashabiki staili za kucheza nyimbo zake zote kali ikiwemo Chura. Pia Kundi la Muziki wa Mwambao la Zanzibar Stars litakuwepo kutoa burudani ya kishindo likiongozwa na Bi Mwanahawa, Zubeda Mlamali, Sabaha Mchacho na wengine kibao,” aliongeza Mbizo.

Mtonyo sasa!

Watoto wote kiingilio kitakuwa sawa na bure kwani getini watapita kwa pesa kiduchu sana yaani shilingi 3,000 tu, huku wakubwa nao sawa na bureeeeeee, yaani 7,000 tu getini unaachiwa huru kabisa umshike mkono R.O.M.A, Darassa, Stamina, Mr Blue, Snura au waimbaji wa Zanzibar Stars.

OVER ZE WEEKEND

Stamina, Darassa Kulipeleka Jiji Dar Live Sikukuu ya Idd Mosi

Comments are closed.