The House of Favourite Newspapers

Rage: Simba SC Inaifunga Mazembe

Kikosi cha timu ya Simba.

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema kuwa, Simba ina nafasi kubwa ya kuifunga TP Mazembe ya DR Congo katika mchezo wao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Simba inatarajia kuvaana na Mazembe Aprili 5, mwaka huu katika mchezo wa hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo wataanzia nyumbani kisha kumalizia ugenini Aprili 12.

 

Simba ilifanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuichakaza AS Vita kwa idadi ya mabao 2-1, hivyo inahitaji kujipanga ili kushinda katika mchezo wake huo.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Rage ambaye enzi za uongozi wake Simba aliwahi kucheza na Mazembe na kufungwa mabao 3-2 Uwanja wa Taifa mwaka 2011, amesema Mazembe kwa sasa haitishi kama ilivyokuwa zamani, hivyo Simba wakijipanga kisawasawa wanawapiga.

 

“TP Mazembe ya sasa siyo ile ya zamani, kwa sasa haipo vizuri japo si sana, ukiangalia kwenye msimamo wa ligi yao ipo nafasi ya pili ikiwa imecheza mechi 25 na pointi 58 huku Vita ambao tumewafunga wakiwa wanaongoza ligi wakiwa na pointi 62 wakiwa wamecheza michezo 25.

 

“Ukiangalia mchezo wao wa mwisho walivyokutana, Vita iliifunga TP Mazembe mabao 3-0 na sisi tumewatoa Vita katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, hivyo unaweza kuona jinsi hali ilivyo, Simba ni timu nzuri na ina uwezo wa kufanya vizuri zaidi na kuifunga Mazembe.

 

 

“Kikubwa wachezaji wasibweteke na badala yake wapambane hadi tone la mwisho ili waweze kufanikiwa kushinda mchezo huu, Mazembe ya sasa siyo ile ya zamani, kwa sasa haina sapoti kubwa kama ilivyokuwa huko nyuma kwa kuwa rais wao, Moise Katumbi hayupo DR Congo hivyo kuwa mbali na timu kumesababisha timu hiyo kuyumba, hivyo nguvu ya mwanzo siyo ya sasa,” alisema Rage.

Comments are closed.