The House of Favourite Newspapers

Rage: Yanga Kwa Morrison Wanapoteza Muda Tu

0

MWENYEKITI wa zamani wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amefunguka kuwa Yanga kuendelea kung’ang’ania suala la Morrison kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ni sawa na kupoteza muda kwani hakuna chochote ambacho watapata kwenye kesi hiyo.

 

Rage alikwenda mbali kwa kusema kuwa hakuna sheria yoyote inayosema mshitaki na mshitakiwa wote wanatakiwa kulipia fedha ili kesi yao iweze kusikilizwa na CAS kama ambavyo taarifa ya Yanga ilivyosema wao na Morrison wanatakiwa kuchangia fedha za Kifaransa ‘Franc’ 24,000 kwa maana ya kila mmoja kuchangia Franc 12,000 (zaidi ya Sh milioni 5).

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Rage alisisitiza kuwa: “Kama kweli wametumiwa hiyo barua na CAS ya kulipia hizo fedha waambie wakuonyeshe hizo karatasi, hakuna kitu kama hicho kwamba mshitakiwa na mshitaki wanatakiwa kulipa ada ya kesi yao kusikilizwa. Wanachofanya Yanga ni kupoteza muda tu, hawatapata chochote.“

Nikwambie kuwa kesi zote za CAS zitasikilizwa Januari 12, chukua maneno yangu kesi zote zilizopo CAS zitasikilizwa na hakutakuwa na kesi ya Morrison na Yanga,” alisema Rage.

 

Klabu ya Yanga kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake, Frederick Mwakalebela alisema kuwa wametumiwa barua na CAS wakitaarifiwa kuwa jaji wa kusikiliza shauri lao la kimkataba na Morrison amepatikana na watatakiwa kulipia kiasi hicho cha fedha kabla ya Januari 12, mwakani ili kesi iweze kusikilizwa.

 

Yanga walikata rufaa na shauri lao kulipeleka CAS mara baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kubaini upungufu kadhaa kwenye mkataba wa Morrison ambao alipewa na Yanga, na hadi wakati kesi yake ikiendelea tayari alikuwa amesaini Simba.

Leave A Reply