Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu imewahukumu raia kumi na wanne kutoka nchini Malawi kulipa faini ya shilingi milioni moja kwa kila mmoja ama kutumikia kifungo Cha mwaka mmoja gerezani.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Evodia Kyaruzi baada ya washitakiwa hao kukiri mashatka yanayowakabili ya kuingia na kuishi nchini bila kufuata sheria.
Awali akiwasomea washitakiwa hao Wakili wa Serikali Shija Sitta akisaidiana na Godfrey Ngwijo amedai washitakiwa hao wametenda makosa hayo Juni 21 maeneo ya Mbweni Wilayani Kinondoni Mkoani Dar es Salaam.
Katika shauri hilo mshitakiwa wa kwanza na wanane wamekana shitaka lao moja la kuingia nchini bila kuwa na vibali wakati huo wakikiri kosa la kuishi nchini bila kuwa na nyaraka yoyote ya kuwaruhusu kufanya hivyo ambapo wakili Sitta ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya washitakiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine wasiofuata sheria za uhamiaji.
Miongoni mwa washitakiwa hao waliohukumiwa ni pamoja na George Chirwa, Samwel Kamanga, Edward Kasambara na Francisco Abinara.
Hata hivyo washitakiwa wote wamepelekwa gerezani baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na wamepelekwa gerezani.